Mradi wa Afya kunufaisha vijana 2,500

VIJANA 2,500 wa Rungwe mkoani Mbeya na Mufi ndi mkoani Iringa wanatarajiwa kunufaika na Mradi wa Afya na Ujasiriamali kwa vijana.

Mradi huo unaendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kupitia Mpango wa Kunusuru kaya Masikini (Tasaf III). Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Tasaf, Fariji Mishael alisema mradi huo utawawezesha vijana hao kuweza kupata ujuzi wa shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato.

Akizindua mradi huo, Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla aliupongeza Uongozi wa Tasaf akisema wameonesha mafanikio chanya ya Tasaf III kiasi cha kuwavutia zaidi wafadhili kujiunga na mpango huo kwa kupanua wigo wa wanufaika.

Makalla aliwataka vijana wanaolengwa na mradi mpya katika wilaya za Rungwe na Mufindi kuitumia fursa hiyo kujijengea msingi wa kuja kuwa na maisha bora zaidi ya kaya zao yaliyosababishwa hadi kutambulika kama masikini ndani ya jamii wanazotoka. Naye Katibu Tawala Uchumi na Uwezeshaji mkoa wa Mbeya, Nyasebwa Chimagu aliahidi kuusimamia mradi huo kwa dhati ili uweze kuleta tija na kutoa hamasa ya kufikishwa wilaya zote nchini.