TCRA yaonya matumizi mabaya ya simu

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa rai kwa Watanzania kuacha kutumia vibaya mitandao ya simu na intaneti badala yake waitumie kwa ajili ya kurahisisha harakati zao za kujiletea maendeleo.

Rai hiyo ilitolewa jana na Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Semu Mwakyanjala wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mwakyanjala alisema kuwa licha ya teknolojia ya mawasiliano kukua na kuleta faida kwenye jamii yetu, bado kuna changamoto nyingi hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anatumia vizuri mitandao hiyo kwa faida yake na taifa kwa ujumla.

Pia alibainisha kuwa wapo baadhi ya watu wasiokuwa wazalendo ambao hutumia mitandao hiyo kusambaza taarifa zenye maudhui ya chuki na uchochezi na kuongeza kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.