Siku 10, polisi Dar es Salaam yaingiza bilioni 1/-

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kimefanya msako wa kukamata magari yanayodaiwa faini ya makosa mbalimbali ya usalama barabarani baada ya kuandikiwa katika mfumo wa Traffi c Management System na kushindwa kulipa kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Lazaro Mambosasa alisema msako huo ulifanyika kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 4, mwaka huu.

Alisema msako huo ulifanywa katika mikoa mitatu ya kipolisi na kwa Mkoa wa Ilala jumla ya magari 946 yaliyolipiwa ni 906 huku magari 40 yalipelekwa vituoni kwa kushindwa kulipiwa kwa wakati na jumla ya fedha za madeni zilizolipwa kwa mkoa huo zikiwa ni zaidi ya Sh milioni 100.

Alisema katika Mkoa wa Kinondoni magari 641 yalikamatwa, Magari 607 yalilipiwa huku 34 yakipelekwa vituoni kwa kushindwa kulipia na kiasi cha fedha zaidi ya milioni 61 kikipatikana.

Aliongeza kuwa kwa upande wa Mkoa wa Temeke jumla ya magari 497 yalikamatwa 469 yalilipiwa huku magari 28 yakipelekwa kituoni na kukusanya zaidi ya Sh milioni 78. Aidha Kamanda Mambosasa alizungumzia makusanyo ya makosa mbalimbali ya usalama barabarani na kusema Polisi imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni moja kwa muda wa siku 10.

Alisema fedha hizo zimekusanywa na kikosi chake cha Usalama barabarani kufuatia operesheni inayoendelea ya ukamataji wa makosa ya Usalama Barabarani. Alisema jumla ya makosa yaliyokamatwa ni 41,892, magari yaliyokamatwa ni 39,747, Pikipiki zilizokamatwa 1,379, daladala 14,704, magari mengine binafsi na malori 25,043. Aidha alisema waendesha pikipiki 97 walifikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu (helmet) na kupakia mishikaki.