Wakosa madarasa, wasomea kanisani

SHULE ya Msingi Missuna iliyopo katika Kata ya Ngimu wilayani Singida inakabiliwa na uhaba wa madarasa, hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi wake kusomea kwenye Kanisa lililopo jirani na shule hiyo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Paschal Jacob alisema shule hiyo yenye darasa la kwanza hadi la sita ina vyumba vya madarasa vitatu, hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kukosa nafasi shuleni hapo na hivyo kuomba uongozi wa kanisa kutumia eneo lao kwa ajili ya madarasa.

“Hofu yetu ni kwamba iwapo kutatokea shughuli ya kidini katikati ya wiki, kama vile kufunga ndoa, wanafunzi wetu watalazimika kukosa masomo,” alisema. Aidha, alieleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya walimu kwani ina wawili na wamekuwa wakitumia walimu wa muda ambao hawajapata mafunzo rasmi ya ualimu huku akifichua kuwa hakuna vyoo kwa wanafunzi wala kwa walimu shuleni hapo.

Kutokana na kutokuwepo vyoo, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Iddi Kijida alisisitiza umuhimu wa jamii katika eneo hilo kujenga vyoo kwa ajili ya shule yao.