Museveni atajwa urais Afrika Mashariki

NAIBU Rais wa zamani wa Kenya, Dk Kalonzo Musyoka anatamani kuona Yoweri Museveni (73), mara baada ya kustaafu urais Uganda, awe Rais wa Afrika Mashariki.

Musyoka amemsifu Museveni kwa upendo wa dhati aliyonayo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kwamba, eneo hilo linahitaji Rais mmoja ili kuwa na umoja. Kwa mujibu wa mkataba wa kuanzisha mtangamano wa EAC, miongoni mwa malengo makuu ni kuwa na shirikisho la kisiasa baada ya kuwa na forodha ya pamoja, soko la pamoja, na fedha ya pamoja. EAC ni ushirikiano wa serikali na wananchi takribani milioni 160 wa nchi sita ikiwemo Tanzania, Rwanda, Kenya, Burundi, Uganda na Sudan Kusini. Makao makuu ya jumuiya hiyo yapo jijini Arusha.

“Baada ya kumaliza kutumikia Waganda, Museveni awe Rais wa kwanza Afrika Mashariki. Wote tunajua kwamba Afrika inaelekea kuungana na kitakachotuunganisha sisi ni kuwa na Rais mmoja,” alisema wakati wa mahafali ya Chuo Kikuu cha Teknolojia na Uongozi cha Uganda (UTAMU). Musyoka ni mmoja wa viongozi wakuu wa muungano wa vyama vya siasa vya upinzani nchini Kenya (NASA) na alizungumza kwenye mahafali hayo akiwa Mkuu wa Chuo hicho.

“Museveni ni mmoja wa viongozi Waafrika wenye upendo wa dhati. Tumemuona akipigania amani Kupitia mazungumzo ya amani Rwanda na DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Somalia, Kenya na hivi karibuni kabisa Sudan Kusini,” alisema. Kwa mujibu wa kifungu 5 (2) cha mkataba wa kuanzisha EAC, shirikisho la siasa litaanzishwa katika nguzo kuu tatu ikiwemo ya sera za pamoja za nje na ulinzi.