Marekani, Ujerumani zapinga marekebisho sheria ya uchaguzi

SERIKALI za Marekani na Ujerumani zinayapinga marekebisho ya sheria za uchaguzi nchini Kenya kwa maelezo kwamba ni kinyume cha kanuni bora za utendaji za kimataifa na pia muda hautoshi kumaliza mchakato huo kabla ya Oktoba 26 mwaka huu.

Bunge la Kenya linaendelea na mchakato wa marekebisho hayo yanayoungwa mkono na chama kinachotawala, Jubilee. Mgombea urais kupitia chama hicho, Uhuru Kenyatta amesema marekebisho hayo yatapunguza mashaka na kuongeza uwajibikaji. Mpinzani wake kupitia Muungano wa vyama vya upinzani (Nasa), Raila Odinga anasema, kubadili sheria za uchaguzi wakati huu ni sawa na kubadili sheria za soka baada ya kumalizika dakika 45 za mechi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Msemaji wa Ubalozi wa Marekani, Heather Nauert, marekebisho hayo yataongeza msuguano wa kisiasa na kupunguza imani ya wananchi katika kuuamini mchakato wa uchaguzi.

Hivi karibuni, Marekani ilitoa mwito kwa wanasiasa wanaohusika kwenye uchaguzi wa Rais kuondoka masharti waliyotoa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) likiwemo la kumtaka Ofisa Mtendaji Mkuu, Ezra Chiloba na wenzake tisa waachie ngazi.

Nchi hiyo imeahidi kuunga mkono jitihada za kutafuta mwafaka kwa viongozi na vyama vya siasa na imetoa mwito wahusika washiriki kwa uwazi na kwa nia njema. Ilisema, Serikali ya Marekani ina dhamira ya kusaidia uchaguzi uwe huru, wa haki, unaoaminika kwa kuzingatia Katiba ya Kenya na sheria za sasa. Taarifa hiyo imetoa mwito kwa Nasa kuacha kutoa masharti makubwa kwa IEBC na iiache tume hiyo itekeleze wajibu wake.