Biashara ya Tanzania na Burundi yamkuna Waziri

MAONESHO ya biashara baina ya Burundi na Tanzania yaliyofanyika hivi karibuni jijini hapa, yameikuna Serikali ya Burundi, huku Waziri wa Usafi rishaji na Ujenzi, Jean Bosco Ntunzwenimana (pichani) akisema yamefungua fursa mpya za ushirikiano kibiashara.

“Ni faida kwa wote, lakini naona kabisa Burundi inanufaika na itaendelea kunufaika,” alisema waziri huyo alipokuwa anazungumzia maonesho hayo yaliyofanyika Septemba 30, mwaka huu.

Alitoa mfano kuwa, miaka ya nyuma walizuiwa kutumia Bandari maarufu ya Dar es Salaam iliyopo Tanzania, lakini sasa wanaitumia kupitishia mizigo yao kwa uhuru zaidi, huku wakifurahia huduma za bandari hiyo.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania imewapa nafuu ya kuwaondolea asilimia 40 ya gharama za kusafirisha mizigo kwa njia ya barabara. Aidha, Ntunzwenimana alisema kwa pamoja, Burundi na Tanzania zinaelekeza nguvu katika miradi mikubwa ya ujenzi.

Aliitaja baadhi kuwa ni reli ya Uvinza-Musongati na ule wa barabara ya Bujumbura- Rumonge-Nyanza -Lac -Kasulu -Manyovu. Alisema miradi hiyo imelenga kukuza biashara na ustawi wa maendeleo baina ya nchi hizo, hivyo ni jambo la kujivunia. Akiizungumzia reli ya Uvinza- Musongati, alisema wataalamu wa Burundi na Tanzania watakutana mjini Kigoma Ijumaa wiki hii ili kujadili mradi huo.