Albino kwenye familia hawaleti mkosi’

WATANZANIA wametakiwa kuondokana na dhana potofu kuhusu watu wenye ualbino kuwa wakizaliwa kwenye familia wanaleta mkosi kwenye familia husika na hivyo familia hiyo kutofanikiwa kimaisha.

Hayo yalisemwa juzi mjini Kahama na Katibu wa Chama cha Albino wilaya ya Kahama, Sitta Gillitu, wakati akizungumza katika warsha ya siku moja iliyojumuisha watu wenye Ulbino iliyofanyika kata ya Msalala.

Katibu huyo, alifafanua kuwa watu wenye ualbino ni binadamu wa kawaida kama walivyo watu wengine. Alisema albino ni hali ya mtu kurithi katika familia anayotoka na kuongeza kuwa kupitia mafunzo hayo ambayo yaliwahusisha watumishi wa idara ya maendeleo ya jamii, watendaji wa kata pamoja na vijiji kutoka Halmashauri ya Msalala wanaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa kutoa elimu kwa jamii husika.

“Watu wengi hapa nchini wanadhani kuwa mtu kujifungua mtoto mwenye ualbino ni kama kuzaa mtoto nuksi katika familia, hali hiyo sio kweli bali hali inayotokana na kurithi kutoka katika familia anayotoka na si vinginevyo,” alisema.

Meneja wa Mradi inuishi kwa watu wenye ualbino kutoka Mwanza, Florence Rugemarila alisema kuwa Chama cha wenye Ualbino nchini (TAS) kimekuwa na changamoto nyingi, zinazowakumba ikiwemo kutokuwa na takwimu halisi za watu hao.

Alisema katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, kulikadiriwa kuwepo kwa albino 16,000, idadi ambayo mpaka kufikia sasa imekuwa ikileta sintofahamu huku wengine wakisema idadi hiyo ni ndogo kulinganishwa hali halisi iliyopo.

Aidha, Meneja huyo alisema kuwa mradi huo wa watu wenye ualbino kwa Kanda ya Ziwa, unafanyika katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu na Kagera. Katika Mkoa wa Shinyanga unafanyika wilaya za Shinyanga na Kahama katika Halmashauri ya Msalala. Utadumu kwa miaka miwili na nusu.