Wanaotumia muda mwingi kwenye chai kutumbuliwa

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amewataka watumishi wa umma kuepuka tabia ya kutumia muda mwingi kunywa chai na kusababisha kuchelewa kuwahudumia wananchi, vinginevyo watachukuliwa hatua kali.

Pia amezitaka ofisi za umma kufungua migahawa katika maeneo ya ofisi hizo iwapo hawawezi basi watangaze zabuni kwa ajili ya kuwasaidia wafanyakazi kupewa huduma haraka na kwa wakati. Mkuchika alisema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa Idara za wafanyakazi wa wizara hiyo, baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Angella Kairuki ambaye kwa sasa ni Waziri wa Madini.

Mkuchika alisema, kumekuwa na tabia ya watumishi wa umma kutumia muda mwingi wa asubuhi kunywa chai, hali inayowakwamisha wananchi kuendelea na kazi nyingine kwa kuwa wanatumia muda mwingi kusubiria huduma.

Alisema, hali hiyo husababisha wananchi hasa wanaotokea maeneo ya mikoani, kulazimika kutumia gharama kubwa zaidi kujikimu kwa kuwa wengine wanalazimika hata kulala mijini kutokana na kungojea huduma kutokea ofisi za Umma.

Alisema, wananchi wanayo haki kupewa huduma kwa muda mrefu kutokea ofisi za umma na watumishi wa umma ni wajibu wao kutoa huduma kwa wakati na kila muda, hivyo wanaoenda kunywa chai na kupoteza muda watachukuliwa hatua watakapobainika kupoteza muda.

Alisema, kushindwa kuwahi kutoa huduma kunasababishwa na mambo mengi mojawapo likiwa ni hilo la kunywa chai, lakini pia muda mwingine ni hata migahawa yenyewe ipo mbali kwa hiyo aliwataka kutolewa huduma hiyo kwa kujenga migahawa kwenye ofisi kwa ofisi ambazo hazina migahawa hiyo.

“Hili sio kwa chai tu bali hata pia katika milo yote ni kwa nini mtumishi wa umma utumie muda mwingi kunywa chai au hata kula tu ilhali kuna watu wanangojea huduma, hili halikubaliki na ninaagiza wakuu wote wa Idara kuanzia Wizara, Ofisi za Serikali na Taasisi za Umma kukabiliana na suala hili,” alisema Mkuchika.

Kuhusu rushwa Mkuchika alisema kuwa wananchi wamekuwa wakilalamikia kuwepo kwa suala la rushwa kwenye jamii, ambapo limewakwamisha kwa kiasi kikubwa kupata haki zao. Alisema, wakuu wa idara wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanapingana na rushwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uwepo wa elimu bora kwa watumishi wao katika kukabiliana na rushwa.

Alitoa pia tamko kuwataka maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuhudhuria kongamano mbalimbali zenye lengo la kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na rushwa.

Alisema kuwa atawasiliana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Professa Joyce Ndalichako ili elimu ya kukabiliana na rushwa itolewe kuanzia ngazi ya Shule za Msingi, Sekondari hadi vyuo ili taifa liwe na vijana walioandaliwa vema kukabiliana na rushwa.

“Mimi hili suala linanikera sana la rushwa najiskia hata kutaka kulia nikisia kuwa kuna mtu ameshindwa kuhudumiwa katika hospitali kwa sababu ya kushindwa kutoa rushwa na nitapambana nalo hadi mwisho”alisisitiza Mkuchika.

Kairuki akabidhi ofisi Kwa upande wake, Waziri Kairuki alimtaka Mkuchika kuendeleza nia ya Rais ya kukabiliana na ufisadi na hasa suala zima la watumishi hewa serikalini, ambapo alisema kuwa bado kuna kazi kubwa.

Alisema, licha ya kuwa tayari watumishi hewa wameshafukuzwa na kuchukuliwa hatua kali lakini kuna haja ya kuendelea kuwa na macho na sakata hili kwa kuwa bado watakuwapo wengine mahali.

Pia alisema kuwa kwa sasa takribani watumishi wa umma 40,000 wamedanganya umri wao wa kuzaliwa ambapo hayo yamebainishwa katika uandikishwaji wa vitambulisho vya uraia.

Alisema, wapo watumishi wa umma ambao majina yao katika data za serikali ni tofauti na walizoandika kwenye uandikishaji wa vitambulisho vya utaifa na hiyo inaashiria kuwa wamedanganya umri wa kuanza kazi na kumtaka Mkuchika kuwashughulikia.

“Mimi nakushukuru Mkuchika kwa kuwa uliniachia mikoba katika Wizara hii na kunielekeza kazi na kwa sasa ninaondoka na kukuachia wewe mikoba, ni imani yangu kuwa kwa kuwa wewe ni umekuwa mtumishi wa umma muda mrefu hii Wizara utaimudu zaidi na zaidi,” alisema Kairuki.

Rais John Magufuli alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na katika mabadiliko hayo kwa sasa Mawaziri ndio wanakabidhi ofisi walizoziacha huku wengine wakikabidhiwa.