Mangariba 63 waacha ukeketaji watoto

KATIKA kilele cha siku ya mtoto wa kike duniani, jumla ya mangariba 63 wameelezwa kuacha kufanya kazi ya ukeketaji kwa watoto na kuanza mafunzo ya ujasiriamali utakaowasaidia kujiongezea kipato zaidi.

Mkurugenzi wa Shirika la Kutokomeza ukeketaji Tarime, Stella Mgaya alisema hayo jana wilayani hapa wakati akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo Cha Ualimu.

Alisema kupitia shirika hilo wameweza kuelimisha wasichana 2,166 ili kupata elimu kuhusu madhara ya ukeketaji na kuweza kuepushwa katika vitendo hivyo ambavyo ni vya kikatili.

Kuhusu mangariba, Mgaya alisema kutokana na kutolewa kwa elimu thabiti ya athari za ukeketaji, waliamua kuacha na kuanza kufanya shughuli nyingine ikiwemo za ujasiriamali wa bidhaa mbalimbali zitakazosaidia kujikimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa alisema mkoa huo umeweza kupunguza vitendo vya ukatili kwa watoto kwa kiwango kikubwa kuanzia asilimia 70 hadi 37 iliyopo sasa. Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la Plan International, Martha Lazaro alisema ndoa na mimba ni vitendo vya ukatili kwa afya ya mtoto wa kike.