Alhad akemea wanaomtusi Rais mtandaoni

MWENYEKITI wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Dar es Salaam, Shehe Alhad Mussa Salum amekemea wale wanaotumia mitandao ya jamii kumtukana rais na kusisitiza wanaofanya hivyo wanawatukana Watanzania pia.

Aidha, alimpongeza Rais John Magufuli kwa juhudi za kuifanya Tanzania yenye maadili kwa kupambana na dawa za kulevya, ufi sadi, wizi na ubadhirifu. Hayo alisema wakati wa warsha ya siku moja ya kamati ya amani ya viongozi wa dini Dar es Salaam, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa lengo la kuwaelimisha matumizi salama ya mitandao.

Alisema si vyema kwa kiongozi wa nchi, kutukanwa kwenye mitandao, kwani kufanya hivyo wanatukanwa Watanzania waliomuweka madarakani. Alisisitiza kuwa jambo hilo halikubaliki. “Simu yako ndiyo pepo yako na ndiyo moto wako, ukitumia vibaya bila shaka itakupeleka motoni,” alisema. Alisema viongozi wa dini, makanisa na misikiti wanatakiwa kufanya kazi ya Mungu kwa kuwaokoa watu kwa kuwaelimisha na matumizi sahihi ya mitandao.

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Joshua Mwangasa aliwataka viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao kuhusu matumizi bora ya mitandao ya kijamii ili kuepuka kuvunja sheria ya makosa ya kimtandao kwa kuzingatia maadili na utu. Mwangasa alisema vita dhidi ya uhalifu wa kimtandao ni ya kila Mtanzania. Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema mamlaka hiyo inashirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu ya matumizi bora ya mitandao ili kuifahamu na kuisimamia vema Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2016.