Mwakyembe atoa maagizo mazito Bodi ya ushauri TSN

WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameitaka Bodi mpya ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), kuhakikisha kampuni hiyo inaendelea kukua na kuwa mfano nchini na nje ya mipaka ya nchi.

Pamoja na hayo, Kampuni hiyo ya TSN imebainisha mbele ya waziri huyo mipango na mikakati yake ya kuhakikisha kampuni hiyo badala ya kuwa kampuni ya magazeti pekee, inakuwa kampuni inayotoa huduma za habari nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe alisema ni vyema bodi hiyo ikahakikisha kampuni hiyo iliyodumu sokoni kwa muda wa miaka 88, inakua na kutanua huduma zake, kama ambavyo mpango wa miaka wa mitano wa kampuni hiyo unavyojieleza.

Alikiri kuwa kampuni hiyo ya TSN imefanya mabadiliko makubwa tofauti na miaka ya nyuma kutokana na kujipanga kufanya biashara na kuleta ushindani na mabadiliko katika soko la habari nchini.

“Mchango wenu katika kuibua fursa hasa mikoani umeanza kuonekana, sasa hivi kila mkuu wa mkoa ananyoosha kidole akitaka kufikiwa na kampuni hii. Sasa hivi kuna timu nzuri nina imani TSN hii itapiga hatua sana huko mbele,” alieleza.

Alisema TSN inayochapisha magazeti ya HabariLeo, Daily News na SpotiLeo kwa sasa inafanya vizuri sokoni kutokana na uandishi wake unaozingatia maadili na weledi wa uandishi wa habari.

Aliwataka wajumbe hao wa bodi kutumia uzoefu na taaluma zao wakiwemo wachumi, wanahabari na wanasheria katika kuijengea ufanisi na weledi kampuni hiyo izidi kuwa mfano kwa utendaji na utoaji huduma bora.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu mstaafu Ofisi ya Rais (Utumishi), Hab Mkwizu, pamoja na kumshukuru Rais John Magufuli kwa kumuona na kumpatia wadhifa huo, aliahidi kuwa bodi hiyo itafanya kazi yake ipasavyo kama inavyotarajiwa.

Alisema kwa kuwa hiyo ni kampuni ya Serikali, atahakikisha bodi hiyo inafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa. Alisema kutokana na sifa za wajumbe wa bodi walioteuliwa kuongoza bodi hiyo ya TSN, anaamini itawajibika kwa kuzingatia taaluma, utaalamu, weledi, uadilifu, uwajibikaji na uwazi, ufanisi na uzalendo kwa maana ya kujali maslahi ya umma, watanzania na taifa kwa ujumla.

Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji na mikakati ya kampuni hiyo, alisema kampuni hiyo imejipanga kutoa huduma bora ya habari na si kujikita katika uzalishaji wa magazeti pekee.

“Tunataka tuwe kampuni bora ya Afrika Mashariki. Tunataka mtu yeyote akitaka habari aifikie kwanza TSN. Tumejipanga kutoa habari za uhakika kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazoendana na wakati, hatutaki kufa tunataka kuilinda heshima hii ya miaka 88,” alisisitiza. Alisema tayari kampuni hiyo, imepiga hatua kiteknolojia ambapo kwa sasa ipo katika mitandao mbalimbali ya kijamii kama vile Instagram, twitter na YouTube.

Pamoja na mwenyekiti wa bodi hiyo Mkwizu, wajumbe wengine wa bodi ni Meneja Mawasiliano kwa Umma katika Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo; Mhasibu Mkuu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Melchizedec Hango na Mkurugenzi Msaidizi Rasilimaliwatu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Teddy Njau. Wajumbe wengine ni Mkurugenzi Msaidizi Mipango na Bajeti Mahakama ya Tanzania, Erasmus Uisso; Ofisa Sheria Mwandamizi Mamlaka ya Bandari (TPA), Mutabuzi Lugaziya; Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi na Dk Yonazi.