Sisi tutamuenzi Nyerere kwa vitendo -Magufuli

RAIS John Magufuli amesema serikali yake ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuenzi kwa vitendo na si maneno yale yote mazuri yaliyoachwa na baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Aidha amesema kwamba watafanya hivyo pia kwa kuhakikisha amani iliyopo inadumishwa na Watanzania wanapata maendeleo.

Amesema Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi mwenye sifa ya pekee nchini, Afrika na dunia kwa ujumla aliyekuwa mzalendo, asiyekuwa na tamaa, aliyeweka mbele maslahi ya Watanzania, aliyejitolea kwa nchi yake na nchi za Afrika, asiyekuwa mbinafsi, aliyechukulia rushwa na aliyependa usawa kwa wote.

Dk Magufuli aliyasema hayo, Mjini Magharibi Zanzibar jana wakati akizungumza kwenye kilele cha mbio za Mwenye kwa mwaka huu na maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Mwalimu Nyerere jana. “Sisi kama serikali tumejipanga kusimamia na kuienzi misingi mizuri tuliyoachiwa na waasisi wetu.

Natambua kuwa kuvivaa viatu vyao hatutaweza ila tutajitahidi,” alisema Rais Magufuli. Aliwataka Watanzania nao kila mmoja kwa wakati wake akiamua kwa dhati kuyaenzi mambo ya Mwalimu mazuri lazima nchi itapiga hatua katika maendeleo.

Kwa nini tunamkumbuka Nyerere? Dk Magufuli alisema ni wakati sasa wa Watanzania kuanza kujikumbusha na kujiuliza kwa nini kuna siku maalumu ya kumkumbuka Baba wa Taifa na umuhimu wake kwa taifa ni nini.

Alisema pamoja na kwamba wapo watu wanaomfahamu Baba wa Taifa kwa kufanya naye kazi na wengine kumsoma kwenye vitabu ni vyema wakafahamu umuhimu wake na mchango wake kwa taifa.

Alimuelezea kiongozi huyo kuwa alikuwa ni mzalendo, aliyeamua kuacha kazi yake na kujiunga na chama cha TANU kwa ajili ya kupigania uhuru wa taifa lake na pamoja na kuwa na fursa nyingi za kujiendeleza lakini aliishi maisha ya kawaida.

“Leo hii tujiulize ni kiongozi yupi anayeweza kujitolea akaacha mshahara wake kwa maslahi ya Watanzania? Leo hii tunao viongozi wako radhi kulipwa mapesa na kampuni kubwa na kusaini mikataba isiyo na tija kwa taifa na kuisaliti nchi yao.

Majibu mnayo,” alisema. Alisema Mwalimu Nyerere enzi za utawala wake alifanikiwa kuunganisha wananchi wote, aliiunganisha Tanzania na nchi nyingine ikiwemo kushirikiana na hayati Abeid Amani Karume na kuziunganisha nchi za Zanzibar na Tanganyika na kupata taifa la Tanzania.

“Hebu tujiulize vitendo vyetu vya leo vinaweza kuijengea amani nchi yetu, je tuna uzalendo? Nyerere alikuwa na maono na ndiyo maana alipanga mikakati yake ya kuongoza nchi ili kuendana na maono yake,” alisema.

Ataja mafanikio ya Nyerere Alisema kutokana na maono hayo, alianzisha Azimio la Arusha kwa lengo la kuwabana viongozi wanaojilimbikizia mali, alianzisha viwanda ili kupunguza utegemezi wa kununua bidhaa nje ya nchi, Shirika la Ndege la Tanzania lilikuwa na ndege tisa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilijenga nyumba 6,000 za Watanzania.

“Lakini pia aliweka mkazo kwenye elimu kwa kutoa elimu bure bila ubaguzi na alihimiza watu kufanya kazi kwa bidii. Hii ni mikakati aliyojiwekea kujenga taifa alilolitaka. Lakini pamoja na misingi aliyotuachia,” alisema.

Hata hivyo, alisema pamoja na misingi mizuri iliyoachwa na Mwalimu Nyerere, siku chake misingi hiyo ilivunjwa, Azimio la Arusha lilifutwa na viwanda na mashirika ya umma viliuzwa. Na takwimu zinaonesha hadi sasa viwanda vilivyouzwa 197 vimekufa na kubaki magofu.

“Ndiyo maana kila siku nasema na kujiuliza hivi sisi Watanzania ni nani alituloga? Kwa nini tuliuza viwanda vyetu tena vingine vilikuwa vinafanya vizuri tu, ndege zetu zimeenda wapi? NHC kwa nini haijengi nyumba za wanyonge?” alihoji.

Alisema serikali ya awamu ya tano imeendelea kutekeleza misingi aliyoiacha Mwalimu Nyerere ikiwemo suala la kuhamia Dodoma ambapo kwa sasa takribani wizara zote zimehamia katika Makao Makuu hayo ya nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais imebakisha miezi miwili ihamie na Ikulu itahamia mwakani.

Pamoja na hayo alisema wanarejesha misingi ya Mwalimu kiuchumi kwa kujenga uchumi wa viwanda ifikapo 2025 ambako alisema tangu serikali hiyo iingie madarakani ilikuta jumla ya viwanda 49,243 lakini sasa vimeongezeka na kufikia 52,549. Viwanda vipya vikiwa ni 3,306.

Aidha alisema serikali hiyo imenunua ndege sita, mbili tayari zimewasili na nyingine zitawasili muda wowote kuanzia sasa huku ikiamua kutekeleza mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler Gorge utakaozalisha megawati za umeme 2,100 ambapo kwa sasa Tanzania nzima inazalisha megawati za umeme 1,500.

Kukamilika kwa mradi huo kutawezesha nchi kuzalisha megawati 3,600. “Pia tutapanua wigo wa kuboresha huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji na miundombinu. Tumeanzisha mkakati wa kusimamia rasilimali za nchi kama vile madini, misitu, wanyama, maziwa na bahari.

“Naahidi serikali yangu kamwe haitakubali rasilimali hizi ziwanufaishe wachache,” alisisitiza. Mafanikio yaonekana Alisema katika mikakati ya kulinda rasilimali tayari mafanikio yameanza kuonekana ambapo kwa upande wa madini, madini ya almasi uzalishaji wake umeongezeka kutoka karati 18,808 Februari mwaka huu hadi karati za almasi 32,733 Agosti mwaka huu.

Aidha, alisema hali ya uchumi inaendelea kuimarika na lengo la uchumi kukua kwa asilimia 7.1 linazidi kufikiwa, huku bidhaa mbalimbali zikishuka bei na mfumuko wa bei ukipungua.

“Wale wanaoendelea kulalamika kuwa hali inazidi kuwa ngumu si kweli na uchumi unashuka si kweli. “Kinachotokea kinatokana na mabadiliko ambayo hapo baadaye yatanufaisha wengi.

“Ni kweli ukimbana fisadi aliyekuwa ananunua chakula, anapanda bodaboda na anayenunua maji njiani, ni wazi hutamuathiri peke yake bali wale wote waliokuwa wakimtegemea,” alisema. Aliwataka Watanzania wawe wavumilivu kutokana na ugumu wa hali ya sasa kwani hapo baadaye hali itatengemaa na maisha yatakuwa mazuri.