‘Mwenge ni tunu utalindwa’

RAIS John Magufuli amesema kamwe haitotokea katika utawala wake kuzifuta mbio za Mwenge wa Uhuru, kutokana na umuhimu wake katika kuhamasisha maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na kubeba historia na alama ya taifa la Watanzania.

Aliyasema hayo Mjini Magharibi Zanzibar jana wakati wa kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema Mwenge wa Uhuru ni moja ya tunu za nchi zilizoasisiwa na Baba wa Taifa kwa lengo la kuwaunganisha Watanzania, kulinda mipaka ya nchi, kusambaza upendo lakini pia kusimamia maendeleo.

“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema Sisi (Watanganyika), tunataka kuuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau.

Maneno haya yamejaa falsafa nzito ya kujenga taifa la amani, linalojitegemea na linalojali haki,” alisema Rais Magufuli. Alisema Desemba Mosi, 1961 Mwenge huo uliwashwa na kupandishwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro kwa lengo ka kumulika nchi nzima na kuharibu mabaya yote dhidi ya Tanzania lakini pia kujenga mema ya taifa hilo.

Alisema licha ya dhana hiyo njema ya kuwashwa kwa Mwenge huo, bado wapo baadhi ya watu wanaoupinga wakitaka ufutwe. “Nawashangaa sana watu hawa na huwa najiuliza wanatokea sayari gani? Ni Watanzania kweli hawa na je wanaijua vyema kweli historia ya nchi yao?” alisema.

Alisema mtu yeyote anayeifahamu historia ya Tanzania kamwe hawezi kuupinga na kutaka Mwenge wa Uhuru ufutwe. “Sasa mimi katika serikali yangu na ya Dk Ali Mohammed Shein, hatuwezi kukubali Mwenge huu ufutwe kwenye utawala wetu.

Nawaombeni wapuuzeni na muwazomee wanaosema ufutwe,” Alitaja sababu za kutofutwa kwa Mwenge huo kuwa umekuwa ni kichocheo cha maendeleo kwani kwa miaka miwili ya utawala wake pekee, tangu uwashwe Mwenge huo, jumla ya miradi 6,838 yenye thamani ya Sh trilioni 2.51 ilizinduliwa na kuwekewa jiwe la msingi.

Akizungumzia maadhimisho ya wiki ya vijana, Magufuli aliwataka vijana nchini wajitokeze kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa kwa kuwa wao ndiyo injini na nguvu kazi ya taifa hilo.