Mahindi yalundikana Rukwa, gunia lauzwa shilingi 35,000

SERIKALI imeiagiza bodi ya mazao mchanganyiko nchini, kutafuta fedha zitakazotosha kununua ziada ya mahindi mkoani Rukwa, yaliyolundika kwa wakulima.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfan Haule wakati akizindua rasmi msimu wa kilimo 2017/18 katika sherehe zilizofanyika katika Kata ya Mpui wilayani Sumbawanga.

Aidha aliagiza kukamatwa kwa wakala watakaouza pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na mbegu bora za mahindi kwa kukiuka bei elekezi, sambamba na watakaobainika kuuza pembejeo feki za kilimo.

Aliongeza kuwa Serikali mkoa wa Rukwa, imetuma maombi Serikalini kumuwezesha kifedha Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) Tawi la Sumbawanga ili aweze kununua kati ya tani 10,000 hadi 30,000 za mahindi kutoka kwa wakulima, ambapo kilo moja ya mahindi ainunue kwa Sh 500.

“Hii yote ni jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa mkulima wa mahindi mkoa wa Rukwa anakuwa na soko la uhakika na lenye tija , badala ya sasa ambapo gunia la mahindi lenye uzito wa kilo 100 linauzwa kwa Sh 35,000 bei mabayo si rafiki hata kidogo kwa mkulima.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Apolinary Macheta aliitaka Serikali mkoa wa Rukwa, ialike wilaya na mikoa yenye uhaba wa chakula, waje kununua mahindi kutoka kwa wakulima kwa bei ya ushindani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nyangi Msemakweli alieleza kuwa wakulima mkoani humo katika msimu huu ,wameweza kuvuna tani 413,142 za mahindi, ambapo NFRA imepangiwa kununua tani 3,000 tu za mahindi.

Serikali kununua mahindi Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mathew Mtigumwe akihojiwa na Habari Leo jana alisema kuwa Serikali itaendelea kununua mahindi hayo kutoka kwa wakulima, lakini pia wafanyabiashara wa ndani nao wanaweza kwenda kununua na kupeleka kwenye mikoa ambayo ina upungufu wa chakula.

Mtigumwe alisema kuwa msimu uliopita wa kilimo, serikali kupitia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula ilinunua tani 3,000 za mahindi kutoka kwa wakulima katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Sumbawanga na Makambako mkoani Njombe.

Alisema kwa kuwa bajeti waliyonayo, haitoshelezi kununua mahindi yote kwa wakati mmoja, lakini serikali itaendelea kununua mahindi kila wanapopata fedha. Kuuza mahindi nje Ili kudhibiti uuzwaji wa mahindi nje ya nchi, Mtigumwe alisema kuwa serikali imeruhusu wafanyabiashara na wakulima kuuza nje ya nchi unga na siyo mahindi.

Alisema kuuza mahindi nje ni kupoteza ajira kwa wananchi, lakini pia kuzinufaisha nchi hizo kwa kupata bidhaa nyingine zinazotokana na nafaka hiyo ikiwemo pumba. Mikoa yenye upungufu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo alisema kuwa mikoa yenye upungufu wa chakula ni mikoa ya Kanda ya Ziwa, Arusha, Manyara na baadhi ya mikoa ya Kanda ya Kati, ambako serikali ilipeleka jumla ya tani 17,500 za mahindi.

Alisema mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa na mingine huwa wanapanda mahindi mwezi wa Oktoba na Novemba na kuvuna mwezi wa Februari au Machi, lakini kutokana na matatizo ya hali ya hewa, hawakuweza kupata mavuno ya kutosha, hivyo serikali ikaamua kuwasaidia tani hizo za chakula.

Hali ya chakula nchini Kwa mujibu wa Mtigumwe, hali ya chakula nchini ni nzuri kwa kuwa Taifa limejitosheleza kwa asilimia 120. Alisema kwa mwaka jana utoshelevu ulikuwa asilimia 122.

Kutokana na utoshelevu huo, Mtigumwe alisema wananchi wasiwe na hofu kwa kuwa chakula kipo cha kutosha, ingawa kuna changamoto tu ya usafirishaji kwenye baadhi ya maeneo kutokana na ubovu wa barabara. Imeandaliwa na Peti Siyame (Sumbawanga) na Matern Kayera (Dar)