Saratani sasa tishio

IMEELEZWA kuwa tatizo la saratani hapa nchini ni kubwa, ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki, huku inakadiriwa kwa mwaka wagonjwa wapya zaidi ya 50,000 wanagundulika nchini.

Aidha, imeelezwa pia kuwa saratani inazoongoza hapa nchini ni saratani ya mlango wa kizazi kwa asilimia 34, ambayo huwapata wanawake. Akizungumza na HabariLeo jana, Kaimu Mratibu Saratani ya Afya ya Uzazi kutoka Wizara ya Afya Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto, Dk Safina Yuma alisema kuwa idadi hii inakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020.

Dk Yuma alitaja saratani nyingine kuwa ni ya ngozi asilimia 13, ya matiti asilimia 12, ya mfumo wa njia ya chakula asilimia 10, ya kichwa na shingo asilimia 7, ya matezi asilimia 6, ya damu asilimia nne, ykibofu cha mkojo asilimia tatu, ya macho asilimia mbili na tezidume asilimia mbili.

“Saratani ya mlango wa uzazi kwa akina mama inasababishwa na kirusi anayejulikana kama ‘Human Papilloma’ ambaye anasambazwa kwa njia ya kujamiiana. Kirusi hicho kisipodhibitiwa mapema huwa kinasambaa mwilini na kusababisha madhara makubwa ya kiafya kwa mwanadamu,” alieleza Dk Yuma.

Hata hivyo, alisema pamoja na idadi hiyo ya wagonjwa kuwa kubwa, wanaofika kwa ajili ya uchunguzi na matibabu katika Taasisi ya Saratani Ocean Road iliyoko Dar es Salaam ni 5,000, wengi wakiwa katika dalili za mwisho za ugonjwa huo ambapo kutibika inakuwa siyo rahisi.

Aidha, alisema idadi hiyo ya wagonjwa wapya wanaofika katika Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa ajili ya kupata tiba ni asilimia 10 tu. “Asilimia themanini ya wagonjwa hao wanafika hospitali ugonjwa ukiwa tayari katika hatua za mwisho,” alieleza Dk Yuma.

Dk Yuma alisema kuwa tafiti zinaonesha kuwa ifikapo mwaka 2035, tatizo la saratani litaongezeka kwa asilimia 50 duniani kote kama hatua madhubuti za kuukabili hazitachukuliwa mapema.

Aidha, Dk Yuma alisema kuwa Oktoba umechaguliwa kimataifa kuwa mwezi wa kuhamasisha jamii kuhusu saratani ya matiti. Alisema lengo la uhamasishaji huo kwa kupitia njia mbalimbali, ikiwemo vipeperushi na mabango ni kuwafanya wananchi kujua dalili hatarishi za saratani ili waweze kuchukua hatua mapema.

Katika kuhakikisha watoa huduma katika hospitali za wilaya, mikoa na kanda, wanakuwa na uelewa mzuri wa maradhi hayo wawasaidie wananchi, Dk Yuma alisema kuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inatengeneza miongozo mbalimbali ya kuwajengea uwezo ili kuzijua dalili za ugonjwa kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, idadi ya wagonjwa wa saratani ya mlango wa uzazi, saratani ya ngozi na saratani ya matiti, waliofika kwa matibabu Taasisi ya Ocean Road tangu mwaka 2005 hadi 2015.