‘Hakutakuwa na darasa nchini lililoezekwa nyasi ifikapo 2020’

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Tano imepania kuwa mpaka kufi kia mwaka 2020, hakutakuwa na darasa nchini lililoezekwa kwa nyasi.

Profesa Ndalichako alisema hayo wakati alipotembelea wilaya ya Korogwe akitokea Tanga mjini mwishoni mwa wiki iliyopita. Alitembelea na kukagua baadhi ya shule za msingi na sekondari za mjini Korogwe, ambazo majengo yake yamejengwa kwa uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na wananchi.

Alisema serikali ipo kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii, ambapo kwa upande wa elimu itaboresha miundombinu kwa kujenga majengo bora na imara.

“Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuboresha miundombinu ya elimu nchini na mpaka kufikia mwaka 2020 hakuna darasa litakalokuwa limeezekwa kwa nyasi,” alisema Profesa Ndalichako.

Aliwataka walimu kuwa wazalendo kwa kuwafundisha wanafunzi uzalendo wa kuipenda nchi yao na kwa kufundisha kwa weledi. Aliipongeza halmashauri ya wilaya ya Korogwe kwa kuwashirikisha wananchi katika ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari na mabweni ya shule za sekondari. Alitaka wilaya nyingine nchini kujifunza kutoka Korogwe.