Kenyatta: Hakuna Serikali ya mseto

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto wamesisitiza hakuna mgogoro wa kisiasa nchini humo na hawahitaji mtu kutoka nje kwenda kusuluhisha.

Wamesema pia kwamba, hakutakuwa na majadiliano kwa lengo la kuundwa kwa Serikali ya mseto. “Tunamwambia rafiki yetu Raila (Odinga), hatutajali umetembelea majiji mangapi. Hakutakuwa na majadiliano tena kuhusu serikali ya mseto, mjadala pekee utakuwa na Wakenya kwa kupiga kura,” alisema Ruto.

Walitoa msimamo huo kwenye mikutano ya kampeni kwenye maeneo la Kenol katika Kaunti ya Murang’a na Ndumberi katika Kaunti ya Kiambu. Wakati wa mkutano Kenol, Kenyatta alisema nchi hiyo haihitaji wasuluhishi kwa sababu haipo kwenye mgogoro.

“Hatutaki usuluhishi au kukutanishwa. Kofi Annan hayupo Kenya. Apande ndege arudi (Odinga) nchini kuomba kura,” alisema na kumtuhumu mpinzani wake kuwa anatafuta kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kwa kujenga mtazamo kuwa demokrasia nchini humo imeoza.

Kenyatta alisema wazungu hawawezi kuitawala nchi hivyo, kama Raila anautaka urais arudi kwa Wakenya. Wakati wa mkutano wa kampeni kwenye eneo la Ndumberi, Kenyatta alisema Kenya inaongozwa kwa kuzingatia sheria na Katiba ambayo haina ibara inayohusu serikali inayotokana na majadiliano.

“Kwenye Katiba yetu hakuna ibara inayoruhusu watu wa nje kusimamia mambo ya taifa letu. Chini ya Katiba yetu ni Wakenya tu wenye haki kuamua akina nani wawe viongozi wao,” alisema na kuongeza kuwa Raila anataka kutumia mlango wa nyuma apate madaraka, lakini Wakenya hawatamruhusu.

“Hakuna mtu, jeshi au nchi inayoweza kumpa mtu uongozi wa nchi. Mtu pekee anayeweza kutoa hiyo fursa ni Mungu kupitia Wakenya,” alisema na kumtuhumu mpinzani wake kuwa anachafua sifa ya nchi hiyo nje ya nchi.

“Kama wanataka (nchi za nje) kumsaidia, msaada bora wanaoweza kumpa ni kumkatia tiketi ya ndege arudi Kenya aanze kampeni ili watu wa Kenya waamue Oktoba 26,” alisema Kenyatta kwenye mkutano wa Ndumberi.

“Watu kama Kofi Annan wanakaribishwa Kenya kama watalii na si kuingilia siasa za Wakenya,” alisema kwenye mkutano huo. Kwa mujibu wa Kenyatta na Ruto, Wakenya ndiyo wenye mamlaka ya kuchagua viongozi wao kwa kupiga kura lakini kuna mtu anataka kupata madaraka bila kuzingatia taratibu za Katiba.