Oman yaridhia kusaidia utafiti wa mafuta Z’bar

SERIKALI ya Oman imesema ipo tayari kutoa ushauri na msaada wa kitaalamu katika utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi Zanzibar.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Mohamed bin Hamad Al-Rumhi wakati akizungumza na waandishi wa habari hapo katika uwanja wa ndege wa Karume Pemba.

Waziri huyo alisoma Pemba katika Shule ya Uweleni. Alisema utafutaji wa mafuta unahitaji umakini wa hali ya juu ikiwemo kufanya utafiti katika masuala ya mazingira na athari zake.

Rumhi alisema Zanzibar inayo nafasi kubwa zaidi katika kufanya utafiti wa nishati ya mafuta na gesi ili kuona kasoro ambazo zimejitokeza baadhi ya nchi hazijitokezi kwa upande wao.

“Nimefanya mazungumzo na Waziri wa Nishati wa Zanzibar kuhusu masuala ya utafiti na mashirikiano ikiwemo kutoa ushauri katika masuala hayo... nimewataka waje tuzungumze,” alisema.

Numhi aliyefuatana na ujumbe wa mawaziri na maofisa wa ngazi za juu kutoka Oman ambao wapo ziarani Unguja wakitumia meli ya kifahari ya Mfalme Qaboos bin Said al Said, alisema amefurahishwa na kuwepo kwa taarifa za Zanzibar kuwepo dalili za mafuta na gesi.

Aidha, alifurahishwa na juhudi za kuvitangaza visiwa vya Unguja na Pemba katika sekta ya utalii ikiwa ni juhudi za kukuza sekta hiyo. Akizungumza na kuutakia safari njema ujumbe huo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdallah alisema wamefurahishwa na ujio huo wa viongozi wa juu kutoka Serikali ya Oman ambao walikuja nyumbani kwao kutembea. Aliutaka ujumbe huo kutumia safari ya ziara hiyo kuitangaza Zanzibar katika ramani ya sekta ya utalii nchini Oman.