‘Vidhibiti mimba vinaharibu maadili’

WAZIRI wa Elimu wa Uganda, Janet Museveni amesema, upatikanaji holela wa njia za uzazi wa mpango kwa kiasi fulani unachangia mmomonyoko wa maadili kwenye jamii. Janet ni Mke wa Rais Yoweri Museveni.

Janet alisema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike kuwa maadili yamemomonyoka kwa kuwa watu wana uhuru wa kufanya ngono. Alisema, aliwalea mabinti zake kama alivyolelewa yeye, na kwamba, walisaini ‘mkataba’ wa kutofanya ngono kabla ya ndoa ukawawezesha wakaolewa wakiwa bikira.

Watoto wa Rais Museveni ni pamoja na Diana Museveni aliyeolewa na Geoffrey Kamuntu, Natasha Museveni ameolewa na Edwin Karugire, na Patience Museveni ameolewa na Odrek Rwabwogo.

“Matumizi ya njia za uzazi wa mpango si utamaduni wetu, hatusikii ufahari tena kusema hapana, watu wanapewa vidhibiti mimba watumie na wafanye wanachotaka, wafanye ngono, wanywe vidonge, wapate ujauzito na kutoa mimba, huu si utamaduni wa Afrika,” alisema ”Nilifanya mabinti zangu wote wasaini kadi za ‘penzi la kweli lina subira’ na wangeepuka kufanya ngono hadi usiku wa siku ya kuolewa ili hizo kadi wawaoneshe waume zao,” alisema kwenye mkutano huo wilayani Kyenjojo. Alisema, kwenye jamii aliyokulia, wanajamii walishirikiana kumlea mtoto kimaadili lakini hali sasa ni tofauti.