Kagame ataja siri ya Rwanda kufanikiwa

RAIS wa Rwanda, Paul Kagame amesema ingawa fedha za kuwekeza katika maendeleo ni kidogo, Serikali ikishirikiana na sekta binafsi mafanikio lazima yapatikane.

Alitolea mfano wa nchi yake kuwa inapiga hatua kutokana na kushirikisha sekta binafsi. Aliyasema hayo kwenye makao makuu ya Benki ya Dunia jijini Washington, Marekani katika mhadhara kuhusu namna ya kuongeza fedha za kugharamia maendeleo.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, ili kupata mafanikio, sekta ya umma na sekta binafsi zinahitajiana na kwamba hiyo ni njia mbadala kukabili upungufu wa fedha za maendeleo. “Mafanikio tunayoyatafuta kwenye nchi zote hayawezi kuja kutoka sekta ya umma kivyake au sekta binafsi kivyake.

Lazima zije pamoja, upande wa sekta ya umma ufanye unachoweza kufanya na sekta binafsi ufanye unachoweza na tunapokuwa pamoja tunaweza kuongeza fedha za maendeleo,” alisema Rais Kagame.

Alitoa mfano kuwa, baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda, sekta zote zilikuwa na uwezo mdogo hasa sekta binafsi hivyo serikali ilitafuta namna ya kujaza pengo hilo ikafanya kazi na taasisi za kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia.

“Tulichojifunza kutoka kwenye yote haya ni kwamba, masoko yakiachwa yenyewe haitatatua matatizo yetu. Tunaweza kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali tufanye tunachoweza kufanya kukabili mapungufu yaliyopo kwenye soko.” “ilibidhi utafutwe udhibiti ili kwenye mchakato wa kufanya biashara kuwe na utabiri.

Benki ya Dunia imetunufaisha tumejenga mazingira ya urahisi wa kufanya biashara kwenye nchi yetu,” alisema. Alisema, Serikali ya Rwanda iliwasaidia wadau wa maendeleo wa kimataifa kufanya shughuli zao kwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira ya kuwavutia wawekezaji. “Kuna vikwazo, kwa mfano wawekezaji kule wanaotaka kuwekeza fedha zao popote wanapotaka kuziweka wataangalia hali kama yetu kama soko dogo, “ alisema.