TSN yapongezwa kwa Jukwaa la Biashara Tanga

WAJUMBE wa Kamati ya Ushauri (RCC) Mkoa wa Tanga wamepongeza Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kufanikisha na kufadhili mkutano wa Jukwaa la Biashara uliofanyika Agosti 17, mwaka huu.

Wamesema ubunifu uliofanywa na kampuni hiyo inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo kupitia Mhariri Mtendaji wake, Dk Jim Yonazi, umewezesha wananchi na dunia kwa ujumla kupata taarifa kwa kina kuhusu fursa za uwekezaji zinazoibuka pamoja na taarifa muhimu za bidhaa, biashara na masoko.

Wametoa pongezi hizo wakati wakichangia hoja kwa nyakati tofauti katika kikao cha RCC kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Tanga. Akiwasilisha taarifa ya mkutano huo, Ofisa Maliasili wa Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga, Timothy Sosiya alisema lengo lilikuwa ni kuibua na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo, kuwakutanisha wadau wa maendeleo pamoja na kutangaza shughuli zinazofanywa ndani ya mkoa ili kupanua uwekezaji na masoko.

“Walengwa wa jukwaa hili walikuwa watu 250, lakini tunapongeza juhudi zilizofanywa na kampuni hiyo wa kuwezesha washiriki 330 wakiwemo viongozi wa serikali, taasisi na wajasiriamali kuhudhuria.

Kimsingi kupitia ubunifu huo ulioletwa na TSN, mkoa umepata faida kubwa ikiwemo fursa kwa wadau kutangaziwa habari zao kupitia mitandao ya kijamii ya kampuni hiyo yenye watazamaji zaidi ya milioni moja,” alisema Sosiya na kuongeza: “Pia halmashauri zetu za wilaya na mashirika mbalimbali ya umma weweza kutumia magazeti ya HabariLeo na Daily News kuchapishiwa taarifa kuhusu shughuli zao.”

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Jimbo la Muheza, Balozi Adadi Rajabu alisema kwa kuwa jukwaa hilo limeleta faida, kuna umuhimu kwa viongozi kwa kushirikiana na TSN kuendelea kuboresha katika siku zijazo.

“Faida ya majukwaa uandaaji wa makini kama hili lililobuniwa wa TSN ni kupata wafanyabiashara na wawekezaji makini, ushauri wangu ni kwamba tumeanza vizuri hivyo tuendelee kushirikiana na kampuni hii ili tutakapoanza maandalizi mengine tuweze kualika washiriki wengi zaidi hasa mabalozi pamoja na wafanyabiashara wakubwa, kwetu sisi viongozi wa Tanga tutalazimika kuwafuata na kuwaomba waje kushiriki,” alieleza Balozi Adadi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela aliwaeleza wajumbe kwamba baada ya jukwaa hilo, ofisi yake imeendelea kufuatilia utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyoibuliwa na washiriki, ambayo yatasaidia wajasiriamali kuendelea kupata taarifa za bidhaa, biashara na masoko. Mada zilizowasilishwa kwenye jukwaa hilo zilizungumzia fursa za uwekezaji, uzoefu, mazingira ya ufanyaji biashara, ubora wa huduma zinazotolewa, upatikanaji wa mitaji pamoja na uanzishwaji wa majukwaa ya biashara katika kila wilaya