Oktoba 30 ni mbivu mbichi za Ole Nangole

JAJI Modesta Opiyo wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha anatarajia kutoa uamuzi wa kesi ya maombi ya kukata rufaa nje ya muda iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha kwa tiketi ya Chadema, Onesmo Ole Nangole, Oktoba 30, mwaka huu.

Ole Nangole kupitia mawakili John Mallya na Adamu Jabir, waliwasilisha maombi mbele ya Jaji Opiyo, Septemba 18, mwaka huu na jaji huyo aliwataka mawakili hao kueleza kwa maandishi na kuwasilisha katika mahakama hiyo Oktoba 3, mwaka huu sababu za kukata rufaa hiyo nje ya muda.

Jaji Opiyo alisema Oktoba 10, mwaka huu, mawakili Masumbuko Lamwai, Edmund Ngemela na Daud Haraka wa upande wa mujibu maombi, wawe wamejibu sababu hizo na Mahakama Kuu kufanya majumuisho Oktoba 16, mwaka huu.

Alisema baada ya kupitia maombi hayo na kusoma pingamizi, Mahakama Kuu itatoa uamuzi wa maombi hayo Oktoba 17, mwaka huu. Lakini jana, Jaji Opiyo alisema amepokea maombi na sababu za kupinga kusikiliza maombi hayo na uamuzi wa kesi hiyo kusikilizwa ama kutosikilizwa atayatoa Oktoba 30, mwaka huu.

“Nimepitia maombi yaliyowasilishwa kwa maandishi na pia nimepitia sababu za kupinga kusikiliza maombi haya, sasa uamuzi wa kusikiliza ama kutosikiliza nitatoa Oktoba 30, mwaka huu,” alieleza Jaji Opiyo.

Juni 29, mwaka jana, Jaji Silvangirwa Mwengesi aliyekuwa akisikiliza kesi alimvua ubunge Ole Nangole kwa kile alichoeleza kuwa taratibu za uchaguzi zilikiukwa. Hata hivyo, Nangole hakukubaliana na uamuzi huo na kuamua kukata rufaa katika mahakama hiyo na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Mwenyekiti wa jopo hilo, Jaji Sauda Mjasiri, Jaji Profesa Ibrahim Juma na Jaji Mussa Kipenka walikaa na kuisikiliza rufaa hiyo.

Lakini kabla ya kuanza kuisikiliza rufaa hiyo, mawakili wa mjibu rufaa Daudi Haraka, Ngemela na Dk Lamwai, walipinga kutosikilizwa rufaa hiyo kwa madai kuwa imekosewa kisheria kwa kuwa haikuwajumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Longido hivyo inapaswa kutupiliwa mbali.