Mamia wamuaga Marehemu Rose, Kuzikwa leo

MAMIA ya watu wakiwemo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari jana walishiriki ibada ya kumuaga Rose Athumani (41) aliyekuwa Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo.

Rose alifariki dunia usiku wa Novemba 9, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu. Aliagwa jana katika Kanisa Katoliki la MNH na anatarajiwa kuzikwa leo Kijiji cha Ongoma, Uru Kaskazini, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ibada hiyo iliongozwa na Padri Paulo Chiwangu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Shemasi Raymond Mukhotya, aliyetoa mwito kwa jamii kusaidia watu wakiwa hai badala ya kusubiri wakiwa wamefariki dunia.Mukhotya alisema jamii kwa sasa imekuwa ikijisahau kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali, wakiwemo wagonjwa lakini wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuwasaidia waliokufa.

“Unaweza ukakutana na mgonjwa anatembea na fomu ya kuomba msaada hadi inachakaa mkononi mwake hapati msaada, lakini inapotokea amekufa unaweza kuona mtu anajitokeza hata kununua jeneza peke yake. Mtu akifa anakuwa mzuri kuchangiwa,” alisema Mukhotya. Aidha, alisema kifo ni fumbo la juu kabisa kwa wanadamu na hakizoeleki na kwa Mkristo kifo siyo mwisho, bali ni daraja na safari ya kuelekea nchi ya ahadi.

Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi alitoa pole na kuishukuru familia kwa kuwapatia zawadi ya Rose aliyekuwa rafiki, dada na mfanyakazi wa TSN aliyefanya kazi yake kwa weledi wa taaluma yake. “Kumbukumbu yake itabaki katika maisha yetu, nawashukuru wafanyakazi wa TSN mlivyojitoa na ninawapa mwito tuangalie yale mazuri Rose aliyotuachia iwe hazina katika maisha yetu na hivyo ndivyo tutakavyoweza kumuenzi,” alisema Dk Yonazi.

Naye Mhariri wa Habari wa Daily News, Leonard Mwakalebela alisema Rose alikuwa kipenzi cha kila mtu na alikuwa mchapakazi wa aina yake katika kipindi chote. “Hata alipoanza kuumwa bado alikuwa anakuja kazini, alikuwa anaweza kufanya kazi yoyote, hakatai kazi unayompangia, hachagui kazi, tunasikitika kwa sababu alipenda kazi yake iwe bora ili inapotoka na jina lake aonekane kweli amefanya kazi, hivyo tumepoteza kipenzi, tumepoteza kamanda,” alisema.

Akizungumzia utendaji kazi wa Rose, Mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Kibwana Dachi alisema wamepoteza mwandishi mzuri katika tasnia kwa kuwa alikuwa ni mwandishi mzuri aliyebobea hasa katika habari zake alizokuwa akiziandika na kuchapishwa gazetini.

Ofisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Magreth Chambiri alisema Rose alikuwa mchapakazi na mcheshi na kazi zake zilikuwa ni za kuvutia, hivyo tasnia ya habari imepoteza mwanahabari mahiri na kutoa mwito kwa wanahabari wengine kuiga mfano wa Rose.

Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kuluthum Ali alisema ingawa hakuwa akifanya kazi ofisi moja na Rose, bado alikuwa ni rafiki yake wa karibu, hivyo kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa tasnia ya habari, jamii na mtoto wake ambao wote walikuwa wakimtegemea. Naye Mjomba wa marehemu, Cornelius Kariwa alisema Rose alizaliwa Septemba 22, 1976 Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ameacha mtoto wa kiume, Michael Edward (Brian). “Rose alikuwa mtoto mwema mwenye karama nyingi na tulimkumbatia, alikuwa na bidii nyingi ya kujiendeleza. Tunawashukuru wote walioshirikiana nasi tangu alipougua na katika ibada hii wakiwemo wafanyakazi wenzake,” alisema Kariwa. Rose amepata elimu hadi ngazi ya Chuo Kikuu na aliajiriwa rasmi na TSN mwaka 2009. Hadi mauti yanamkuta, alikuwa akifanya kazi ya Mwandishi wa Habari Mwandamizi na Makala katika gazeti la kila siku la Kiingereza la Daily News.