Muswada kufuta TTCL watua bungeni

MKUTANO wa Tisa wa Bunge unaendelea leo huku miswada minne ikitarajiwa kuwasilishwa ukiwemo wa kutungwa Sheria ya kuanzisha Shirika la Mawasiliano wa Tanzania na kufuta Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Pamoja na mambo mengine, shirika hilo litakuwa na kazi ya kutoa huduma za kiufundi, ushauri na kihandisi kuhusu Tekonolojia ya Mawasiliano kwa taasisi za Serikali. Pia kutawasilishwa Muswada wa kuanzisha Shirika la Wakala wa Meli ambalo litakuwa na jukumu la kutoa huduma za uwakala wa meli na kudhibiti huduma za usafiri na usalama wa vyombo vya majini.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, muswada huo mawasiliano utawasilishwa kesho. Mbali na kutoa huduma hizo kwa taasisi za Serikali, pia itatoa huduma kwa mashirika makubwa na madogo, wajasiriamali wadogo na wa kati na mamlaka nyingine. Muswada wa kuanzisha Shirika hilo la Mawasiliano Tanzania wa mwaka 2017, unaeleza Ofisa Mtendaji Mkuu atateuliwa na Rais na wafanyakazi na mali zote za TTCL zitahamishiwa kwenyeshirika hilo na bila kutozwa kodi.

Vile vile unabainisha kuwa TTCL Pesa itakuwa kampuni tanzu ya shirika hilo la mawasiliano huku ikiendelea na kazi zake za huduma za kifedha. Miswada mingine itakayowasilishwa wiki hii kabla ya kuahirishwa kwa Bunge Ijumaa ni wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017.

Mingine ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4 wa Mwaka 2017 na Muswada wa Marekebisho ya Sheria Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017. Miswada hiyo itasomwa katika hatua zote. Katika muswada wa kuanzishwa Wakala wa Meli, majukumu yake yanatajwa kuwa ni kuhakiki shehena inayoingia na kutoka kupitia bandari za Tanzania.

Mengine ni uondoshaji shehena za madini, makinikia, nyara za Serikali, wanyama hai, bidhaa zitokanazo na madini na udhibiti wa watoa huduma katika sekta ndogo ya usafiri wa majini na usalama wa meli na mazingira ya bahari.

Pia utafanya ukaguzi wa meli za kigeni na udhibiti wa meli zilizosajiliwa nchini, udhibiti wa vivuko vya kibiashara, kudhibiti shughuli za utafutaji na uokoaji, kudhibiti, kuratibu na kulinda mazingira ya habari.

Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, utahusisha Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Sura ya 216. Lengo ni kuondoa utata wa vyombo vya utatuzi wa migogoro ya ardhi katika ngazi ya kata na wilaya ambavyo vinatakiwa kuanzishwa katika mamlaka za wilaya pekee na si mamlaka za miji.

Pia kutakuwa na marekebisho ya kuruhusu baraza la ardhi na nyumba la wilaya kuwa na zaidi ya mwenyekiti mmoja na msajili wa baraza hilo kuwa na sifa ya shahada ya sheria na uzoefu miaka 10. Kwa mujibu wa muswada huo, Sheria ya Upimaji wa Ardhi inayorekebishwa itawekwa kifungu kipya kuruhusu kutambulika na kutumika kisheria kwa michoro yote ya upimaji na ramani iliyotayarishwa kielektroniki.

Katika sheria ya mamlaka ya nchi kuhusu rasilimali za nchi ya mwaka 2017 kutaongezwa rasilimali za madini na mafuta. Pia kutafanyika marekebisho ya sheria ya Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi sura ya 263 ambapo vipengele vinavyozungumzia malipo ya fidia kwa wafanyakazi waliopata ulemavu wa kudumu wa chini ya asilimia 30 ya kila mwezi yataondolewa na sasa malipo hayo ya fidia yatakuwa ya mkupuo.

Mbali na miswada hiyo, leo wabunge watapitisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali mwaka 2018/2019 ambao kwa wiki nzima iliyopita wabunge waliujadili na kutoa mapendekezo yao.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 94 ya Kanuni ya Bunge Toleo la Januari 2016, Bunge lilikaa kama kamati ya mipango ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 639(3)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kujadili na kuishauri Serikali kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Taifa.