Serikali yasema kuna uhuru mkubwa wa habari nchini

IDARA ya Habari (MAELEZO) imesema ina jukumu la kutoa taarifa sahihi za serikali kwa wakati, kusajili na kufungia magazeti pamoja na kusaidia watu katika mifumo mingine ya serikali na utawala nchini.

Pia imeeleza uhuru wa vyombo vya habari upo wa kutosha huku Serikali ikidhihirisha uhuru huo kwa kusajili redio zaidi ya 150, vituo vya runinga zaidi ya 30 huku kukiwa na magazeti zaidi ya 110.

Hayo yameelezwa juzi na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbasi aliposhiriki kwenye kipindi mubashara cha Vijana TZ cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutazama mafanikio, utendaji wa serikali na changamoto katika tasnia ya habari jijini Dar es Salaam. Dk Abbasi alisema serikali ina wajibu wa kuwasimamia na kuwalinda wananchi, ikiwemo kuhakikisha wanapata haki ya kupata habari sahihi na si kulishwa au kupewa habari mbaya.

Akizungumzia vikwazo na changamoto, alisema msimamo wa idara yake ni kuhakikisha habari sahihi zinawafikia watu wote kwa wakati huku waandishi kalamu zao zikiandika kwa weledi, kuzingatia miiko, kanuni na maadili ya taaluma hiyo.

“Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imefanikiwa kuleta mageuzi ya kifikra, kujenga ari na shime ya uzalendo, nidhamu ya kazi, uwajibikaji kwa watu, watumishi wa umma na wananchi,” alisema Dk Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali.

Aidha, alisema Serikali imefanikiwa kujenga msingi ya nidhamu na udhibiti matumizi ya fedha za umma ikiwemo kuzuia safari za nje zisizo na tija. “Hapo nyuma zilitumika Sh bilioni zaidi ya 200 kwa safari za nje wakati sasa zimetumika sh bilioni 25 tu kwa safari hizo na hivyo Serikali kuokoa pesa nyingi.

Pia udhibiti wa kulipa mishahara kwa wafanyakazi hewa zaidi ya 20,000 na kuokoa zaidi ya sh bilioni 238,” alieleza. Alisema watu wanaopiga kelele juu ya mageuzi ya rasilimali za madini, ipo siku watanyamaza wakiona manufaa yako wazi kutokana na uzalendo uliooneshwa katika kushughulikia mikataba ya madini. Aliwahimiza Watanzania kumuunga mkono Rais Magufuli.