Rais Museveni aishukuru Tanzania bomba la mafuta

RAIS wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Museveni ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali kutumia barabara zake kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa mradi husika.

Rais Museveni alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa sherehe za uwekaji jiwe la msingi wa mradi huo kwa upande wa Uganda zilizofanyika Hoima. Awali sherehe kama hizo kwa upande wa Tanzania zilifanyika Chongoleani, Tanga, Agosti 5, mwaka huu, mahali patakapojengwa gati ya kushusha mafuta.

Eneo la Hoima ndipo kitajengwa Kiwanda cha Kusafisha Mafuta kabla ya kusafirishwa Tanga. Pia Hoima ndiyo eneo ambalo mafuta yataanza kusafirishwa kwenda Bandari ya Tanga kabla ya kusafirishwa nje. Rais Museveni alieleza kugundulika kwa mafuta nchini Uganda kumechangiwa na mafunzo yaliyotolewa kwa wataalamu wazawa wa nchi hiyo ambao wamechangia kugundulika kwa mafuta nchini humo.

Aidha, Rais Museveni alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wazazi na wanafunzi kujikita katika masomo ya sayansi ili wasimamie na kuendeleza shughuli za mafuta nchini humo kwa maendeleo ya nchi hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga akizungumza kwa niaba ya Rais John Magufuli, alisifu Jitihada za Rais Museveni katika kuendeleza utafiti bila kukata tamaa na hatimaye kufanikisha ugunduzi wa mafuta nchini humo kwa kuwatumia wataalamu wa ndani.

Balozi Mahiga alimwelezea Museveni ni Rais ambaye ametoa mfano wa kutokubali kushindwa kutokana na namna historia ya utafiti wa mafuta nchini humo ilivyokuwa akisema amekuwa mfano na alama ya namna ya kuwatumia wataalamu wa ndani kuendeleza rasilimali za nchi kufuatia ugunduzi huo.

Alisema manufaa ya ujenzi wa bomba hilo si ya Uganda tu, bali pia Afrika Mashariki na ugunduzi huo umewezesha kupatikana kwa rasilimali ya thamani iliyofichika Bonde la Ufa ambayo inakuwa ya manufaa kwa nchi hizo na Afrika.

“Nimemjua Museveni tangu akiwa kijana mdogo mwerevu, shupavu na mtu mwenye matarajio makubwa na kiongozi thabiti. Katika hili la ugunduzi nashawishika kusema Uganda wana kila sababu ya kujivunia kiongozi huyu. Ni katika kipindi kirefu nchi inaweza kupata kiongozi bora,” aliongeza Dk Mahiga.

Awali Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Irene Muloni alisema ugunduzi huo umewezesha Uganda kupata mwaliko kutoka Jumuiya ya Nchi zinazozalisha Mafuta Duniani (OPEC) wa kuhudhuria mkutano wa nchi hizo kutokana na ugunduzi wa mafuta nchini humo.

Muloni alisema utekelezaji wa mradi huo unatokana na msukumo na dhamira ya dhati ya marais wa Uganda na Tanzania kwa kuhakikisha kuwa mradi husika unatekelezwa na kuongeza utawezesha kupatikana kwa ajira takribani 10,000 wakati wa ujenzi na utawezesha ajira mpya zipatazo 1,600.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba la urefu wa kilometa 1145, ujenzi wa vituo sita, vinne vya kusukuma mafuta na viwili vya kupunguza kasi ya mafuta na ujenzi wa matangi 5 ya kubeba mapipa 500,000 kila moja na ujenzi wa vali 53 za kufunga bomba. Historia ya shughuli za utafiti Uganda inaonesha utafiti wa mafuta nchini humo ulianza mwaka 1939 ukasimama na miaka ya 1950 ukaendelea na kusimama.

Ilipofika mwaka 1986 Rais Museveni aliita timu ya wataalamu kuweka mikakati ya kuendeleza shughuli za utafiti wa mafuta na ilipotimu mwaka 1993 aliteua wataalam ambao walipatiwa mafunzo na hatimaye wakafanikisha ugunduzi wa mafuta hayo. Mradi huo unaojulikana kama Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) utakuwa na urefu wa kilometa 1145, uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku. Nchini Tanzania bomba litapita katika mikoa 8, wilaya 24, vijiji 134 na Uganda mikoa 8 na wilaya 24.

Bomba la EACOP litajengwa na kuendeshwa na Kampuni ya Bomba la Mafuta kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (NOC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni za Mafuta za TOTAL ya Ufaransa, TULLOW ya Ireland na CNOOC ya China.

Kutokana na asili ya mafuta ghafi ya Uganda kuwa na nta na yenye mnato, bomba litahitaji kuwa na joto njia nzima nakufanya bomba la EACOP kuwa refu kuliko yote duniani lenye mfumo wa joto. Njia ya Tanzania ilichaguliwa na Serikali ya Uganda kutokana na kuwa ya gharama nafuu na yenye uimara.