Marais EAC kukutana Kampala

MAANDALIZI ya mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaotarajiwa kufanyika Novemba 29, Kampala nchini Uganda yanaendelea kwa kasi.

Viongozi hao wanatarajiwa kujadili masuala ya miundombinu, fedha za tiba na maendeleo chini ya kaulimbiu ‘Kukuza na Kupanua Mtangamano kwenye Miundombinu na Maendeleo ya Sekta ya Afya kwenye Nchi wanachama EAC’.

Mkutano huo unaandaliwa na Sekretarieti ya EAC ikishirikiana na nchi wanachama wa EAC, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Pia wamo wadau wakubwa wa maendeleo kwenye eneo hilo na wa kimataifa.

Utakuwa mkutano wa kwanza wa viongozi hao kujadili masuala ya afya na wa nne kuhusu kugharamia miundombinu na maendeleo EAC. Mkuu wa Mawasiliano wa Sekretarieti ya EAC, Richard Owora Othieno amesema, mkutano huo utajadili mambo ya manufaa kwa miundombinu na maendeleo ya afya, dhamira ya kugharamia, uwezeshaji kisiasa kutekeleza miradi yao na uwezekano wa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi na maendeleo ya utekelezaji wa miradi.

Amesema wanatarajiwa kujadili maendeleo ya miradi miundombinu bora, ya uhakika, endelevu, imara na inayotolewa haraka ikiwemo ya kieneo na kuvuka mipaka muhimu kwa maendeleo ya uchumi na hali bora za wananchi.

Wakuu hao wanatarajiwa kujadili uwezeshaji haraka wa usafi ri bora EAC kupitia maendeleo ya mifumo inayoingiliana ya usafi ri zikiwemo barabara, reli, mabomba, usafi ri wa maji ndani ya nchi, viwanja vya ndege na bandari za EAC. Othieno alisema mifumo hiyo itapunguza gharama za usafi rishaji, kuokoa muda na kuboresha usafi ri wa vitu vya uzalishaji mali.

Alisema kwenye sekta ya afya wakuu hao wa nchi watajadili namna ya kuwa na uamuzi wa pamoja kuhusu vipaumbele vya uwekezaji katika sekta ya afya kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu, kutekeleza lengo la kumwezesha kila mtu kupata huduma za afya, kuhamasisha uwekezaji vipaumbele vya sekta ya afya na kuongeza ushirikiano ili kuiboresha.

Mkutano wa wakuu wa nchi utatanguliwa na mikutano tofauti ya wawekezaji sekta za miundombinu na afya sambamba na majadiliano ya washirika na wadau wa maendeleo inayotarajiwa kufanyika Novemba 28, Kampala.

Mkutano wa wakuu wa nchi utafanyika sambamba na maonesho ya sekta ya afya na miundombinu yanayotarajiwa kufanyika Novemba 28 hadi Novemba 29 jijini Kampala. Alisema maonesho hayo yatatoa fursa kwa wahusika sekta za miundombinu na afya kuonesha bidhaa za huduma zao zikiwemo zinazotokana na maendeleo ya tafi ti na ubunifu.