Nyalandu kuchunguzwa kwa kuitia serikali hasara

VYOMBO vya dola vimeagizwa kumchunguza Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akidaiwa kuitia hasara Serikali. Vyombo hivyo, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na Jeshi la Polisi, vimetakiwa kumchunguza kutokana na kushirikiana na Kampuni za Uwindaji na kuwapa vitalu vingi kinyume cha utaratibu.

Uamuzi huo ulitolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla wakati akichangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/19 na mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2018/19.

Alisema katika miaka miwili akiwa Waziri Nyalandu aliitia hasara Serikali kwa kutokusanya tozo katika hoteli kubwa nchini za Sh bilioni 32 sawa na Sh bilioni 16 kila mwaka. Alisema mwaka 2014 na 2015, Nyarandu aliisababishia hasara ya kiwango hicho kwa kutotoza tozo katika hoteli mbalimbali nchini.

Dk Kigwangalla alisema watu wanasema anafukua makaburi, lakini ili kufanya kazi vizuri lazima aondoe mitandao ya ujangili iliyokuwepo wizarani kwanza ndiyo afanye kazi. “Katika miaka miwili 2014-15, hakusaini Gazeti la Serikali (GN) kwa ajili ya kukusanya kodi kwenye hoteli mbalimbali nchini kitendo ambacho kimeitia hasara Serikali,” alisema.

Alisema katika kuonesha ukubwa wa tatizo, hata wapinzani hasa, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) alilalamika kama Dk Wilbrod Slaa angepita kuwa rais na Nassari akateuliwa Waziri wa Mambo ya Ndani, angeshughulika kumwondoa Waziri Nyalandu kutokana na utendaji mbovu.

Alisema Nyalandu alikuwa anatumia muda mwingi kustarehe na kusafiri nje ya nchi hasa Marekani na kuishi kwenye hoteli za kimataifa. Dk Kigwangalla alisema Nassari alikuwa sahihi, kwani Nyalandu alikuwa akiishi hoteli ya Serena ambayo ni kati ya hoteli ambazo hakusaini GN yake ilipe tozo au kodi ya hoteli.

Dk Kigwangallah alilieleza Bunge kuwa Nyalandu alikuwa akifanya starehe katika hoteli ya Serena na kusafiri kwa kutumia helikopta ya tajiri, bilionea na mwindaji maarufu wa Marekani katika kampeni za urais mwaka 2015.

Pia alieleza Nyalandu alitoa vibali vya kuwinda katika vitalu vitano kinyume cha sheria na utaratibu wa ugawaji vitalu kwa kampuni ya Mwiba Holdings, Tanzania Game Tracking mali ya tajiri mwenye asili ya Marekani, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na utaratibu. Dk Kigwangalla alizidi kulieleza Bunge kuwa tajiri huyo aliendelea kuwinda licha ya muda kwisha na aliwahi kukutwa na nyara za taifa.

Alisema zama zinabadilika hivyo wakati sasa Nyalandu anatakiwa kuchunguzwa na akibainika kuitia hasara Serikali anatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa alichokifanya. Alisema vitalu vya uwindaji hutolewa Julai hadi Oktoba na kuhoji inakuwaje bilionea wa Kimarekani aliwinda baada ya muda huo kuisha.

Pamoja na kung’oa mtandao wa ujangili wizarani, Dk Kigwangalla alisema bado anaweka mkakati wa kuongeza utalii, vivutio vingine na kuongeza uwekezaji hasa ukanda wa Kusini ambao Serikali imetoa Sh bilioni zaidi ya 300 kwa ajili ya kuimarisha utalii huo.

Mbali ya Nyalandu, mawaziri wengine waliowahi kuongoza wizara hiyo ni Arcado Ntagazwa (1988- 1990), Abubakar Mgumia (1990-1993), Juma Hamad Juma (1999). Wengine ni Juma Ngasongwa (1995-97), Zakhia Meghji (1997-2005), Anthony Diallo (2005-2007), Profesa Jumanne Maghembe (2007-08). Wengine ni Mhandisi Shamsa Mwangunga (2008- 2010), Ezekiel Maige (2010- 2012) Dk Hamisi Kagasheki (2012), Profesa Maghembe (2016-2017) na sasa Dk Kigwangalla (2017).