Magari ya Tanzania, pikipiki Rwanda gumzo

TANZANIA na Rwanda zinazidi kufanya vizuri katika ubunifu na ujenzi wa viwanda vya kisasa ambapo sasa zinatengeneza na kuuza nje magari ya kubeba watalii, malori ya taka na pikipiki.

Kampuni ya Pikipiki Rwanda (RMC) jijini Kigali iliyoanza kutengeneza aina mbalimbali za pikipiki kuanzia katikati ya mwaka huu, imekuwa gumzo na bidhaa zake zimeanza kuvutia wafanyabiashara wa Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na nyingine.

Aidha, Kampuni ya Hanspaul Automechs Limited (HAL) iliyo eneo la viwanda Njiro jijini Arusha imekuwa gumzo kwa kutengeneza magari makubwa ya kubeba watalii maarufu kwa jina la ‘War Bus’ ambayo Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Satbir Hanspaul amesema yanauzwa Kenya, Afrika Kusini na Ulaya pia. PIKIPIKI ZA RWANDA Mkurugenzi wa Mauzo wa Kampuni ya RMC, Luois Masengesho anasema wafanyabiashara mbalimbali wa Tanzania na DRC tayari wamewasilisha maombi kununua pikipiki zao.

“Hadi sasa tumekuwa tukiuza pikipiki kwenye soko la Rwanda lakini watu kutoka Tanzania na DRC wameonesha nia ya kuzinunua,” alisema. Kiwanda hicho kiko Ukanda Maalumu Kiuchumi na kilifungua duka la kuuza pikipiki Mei 2017. Masengesho alisema, hadi sasa kimetengeneza zaidi ya pikipiki 300, na 130 kati ya hizo zimeshauzwa kwenye soko la Rwanda.

RMC inatengeneza aina saba za pikipiki Ingenzi, Indakangwa, Indahigwa, Imparage, Infarasi na Inzovu na kila moja inauzwa kati ya Faranga za Rwanda milioni 1.2 hadi Faranga milioni 3 kwa kuzingatia uwezo wa injini na ukubwa wake zikiwemo za CC250 na CC125. Masengesho amesema walengwa wakubwa wa pikipiki hizo ni wafanyabiashara wa bodaboda, wanaozitumia kwa ajili ya michezo, maofisa wa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali huko.

“Tunashukuru soko limetupokea vizuri na kwa sababu ya mahitaji yaliyoonekana katika nchi hizi (Tanzania na DRC) tunatarajia kuongeza mauzo zaidi na zaidi,” alisema Masengesho. Alisema baadaye mwezi huu pikipiki hizo zinatarajiwa kuwa kivutio kwenye maonesho ya kila mwaka ya bidhaa zinazozalishwa Rwanda. MAGARI YA TANZANIA HAL imesema imebuni na kutengeneza magari maalumu ya kubeba takataka yanayofaa kwa mazingira ya Tanzania na Afrika Mashariki, ikiwemo hali ya hewa, barabara na mfumo wa maisha na hivyo yatadumu kwa muda mrefu.

“Lakini aina mpya ya malori ya kubeba takataka si kwa ajili ya kampuni yetu au kiwanda chetu tu. Kwa kuzingatia viwango vya TBS (Shirika la Viwango Tanzania), wazalishaji wengine pia wanaweza kutengeneza wakitumia utambulisho wa ubunifu wa HAL kama kielelezo,” alisema Mkurugenzi wa HAL, Hanspaul.

Alisema magari ya kubeba takataka na yale ya watalii ni ubunifu wa Tanzania unaozivutia nchi nyingine zikiwemo za Ulaya na magari ya watalii yanayokubalika soko la kimataifa. “Watu wengi hawataamini nchi zenye viwanda vya kutengeneza magari kama Afrika Kusini na zile za Ulaya sasa zinanunua magari kutoka Tanzania, lakini wanafanya hivyo,” alisema.

Magari hayo yenye nembo za Toyota, Nissan na Land Rover yanatengenezwa kwa kutumia mashine za kisasa zikiwemo robot kama ilivyo kwenye viwanda vya magari katika nchi zilizoendelea. HAL ilianzishwa mwaka 2007.

“Tuna kila kitu, mitaji kutoka taasisi za benki, intaneti yenye kasi, mawasiliano ya simu, nguvu kazi ya kutosha na ardhi ya kutosha, tunachohitaji ni watu kubadili mitazamo yao na kugeukia bidhaa zetu nzuri,” alisema Hanspaul. Kenya, Uganda na Afrika Kusini wanatumia ‘War Bus’ kupeleka watalii hifadhi za taifa na kuna taarifa zinazodai kuwa, baadhi ya nchi zinayatumia magari kwenye shughuli za kijeshi.