Wasomi wa mafuta Uganda wamkosha JPM

RAIS Dk John Magufuli ameelezea kuguswa na uzalendo wa wasomi wa Uganda waliofanikisha kugundua mafuta nchini mwao.

Amesema wasomi hao ni watu maalumu si kwa Uganda pekee, bali Afrika, kwani hata Wazungu walishindwa kugundua mafuta nchini humo. Amesema wasomi hao ni wazalendo wa kweli, kwani kutumia usomi wao kwa manufaa ya nchi kunapaswa kupongezwa na kuigwa na wengine. Katika kuonesha alivyofurahishwa na wasomi hao, Rais Magufuli aliamua kuwaombea tuzo kutoka kwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Rais Magufuli alisema hayo wiki iliyopita akiwa Uganda alikofanya ziara ya siku tatu ya kikazi. “Hawa ni maalumu na wa kipekee. Ni wasomi wa Afrika, si Uganda pekee…mheshimiwa Rais Museveni, wape tuzo.

Wazungu walishindwa kubaini mafuta Uganda, wewe ukawapeleka vijana wako kusoma, wakawa wapole na wakarimu, wakarejea nchini mwao na kwa uzalendo mkubwa wakafanya kazi mpaka mafuta yamepatikana wewe ukiwa Rais… “Wamefanya jambo kubwa na la kuigwa na wasomi wengine Afrika. Si kazi ndogo, wanastahili tuzo za kutambua mchango wao mkubwa kwa taifa la Uganda,” alisema.

Kugunduliwa kwa utajiri wa mafuta kunatarajiwa kuipaisha kwa kasi Uganda kiuchumi kuelekea kwenye uchumi wa kati. Juhudi za kuanza kuchimba mafuta hayo yanayokadiriwa kuwa na ujazo wa mapipa bilioni 6 na bomba lake ambalo ni refu kuliko yote duniani yenye mfumo wa kupashwa moto liko mbioni kujengwa ili lisafirishe mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Litakuwa na urefu wa kilometa 1,445 na kipenyo cha inchi 24 litakalopitia wilaya tisa za Uganda na Tanzania likipita katika mikoa minane, wilaya 24, vijiji 134 na vitongoji 210. Linatarajiwa kufanyiwa uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 3.5 (zaidi ya Sh trilioni 7) na kuzalisha maelfu ya ajira katika nchi zote katika kipindi chote cha miaka mitatu ya ujenzi.

Aidha, karibu kila sekta itafaidika na bomba hilo kama makampuni ya usafirishaji, makampuni ya ulinzi, taasisi za kifedha, huduma za kiafya, kampuni za chakula na mahoteli. Mengine ni makampuni ya wataalamu kama wanasheria, wahasibu, wahandisi, wataalamu elekezi na kadhalika, wakulima, wafugaji, wavuvi hadi mama lishe na bodaboda. Bomba litahamasisha ujenzi wa miundombinu kama barabara, reli, uwanja wa ndege na bandari. Kutakuwa pia na miradi ya huduma za kijamii maeneo mengi ambayo bomba litapita, mfano umeme, maji, shule, barabara.