Jeshi la Zimbabwe: Rais Robert Mugabe yuko salama

Jeshi la Zimbabwe limekanusha taarifa kuwa limepindua serikali, likidai kuwa linachukua hatua ya kuwadhibiti wahalifu. Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo katika Televisheni ya Taifa (ZBC), ilisema kuwa jehi halijafanya mapinduzi na Rais Robert Mugabe yuko salama.

Taharuki kubwa ilitawala katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu baada ya milio mikubwa ya risasi kusikika katika maeneo ya Kaskazini mwa Mji Mkuu Harare mapema leo. Jeshi lilitoa taarifa hiyo ikiwa ni muda mfupi baada ya kudhibiti kituo hicho cha ZBC.

Kwa mujibu wa tovuti ya Kiswahili ya BBC, Mwanaume mmoja ambaye alikuwa amevaa sare za jeshi alisema kuwa jeshi linataka kukabiliana na watu ambao wanatenda uhalifu unaoleta madhara ya kijamii na kiuchumi nchini Zimbabwe.

"Wakati tutakapomalzia wajibu wetu, tunatarajia kuwa hali itarudi kuwa sawa" amesema mwanajeshi huyo na kuongeza kuwa Rais Robert Mugabe (93), na familia yake wako salama.

Wanajeshi wakiwa na silaha nzito wameonekana wakijipanga katika maeneo mbalimbali katika mji mkuu pamoja na kuzingira ofisi za Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC). Hali hiyo imeleta wasi wasi mkubwa kuwa lolote laweza kutokea, imeanza hapo jana jioni, ambapo Hata hivyo taarifa zinasema kuwa wafanyakazi wa shirika hilo la utangazaji ZBC, waliambiwa na wanajeshi hao kwamba hawapaswi kuwa na wasiwasi na kwamba uwepo wa vikosi hivyo ni kwa lengo la kulinda eneo hilo.

Chama tawala nchini Zimbabwe (ZANU – PF kimemtuhumu mkuu wa majeshi Constantino Chiwenga, kwa hatua yake ya madai kuwa jeshi lipo tayari kuingilia mzozo huo wa kisiasa kwa lengo la kulinda wapigania uhuru wa taifa hilo.