Kiongozi wa Umoja wa Vijana ZANU - PF aliangukia jeshi

Kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama tawala nchini Zimbabwe, ZANU – PF, Kudzai Chipanga amemuomba radhi Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Jenerali Constantino Chiwenga baada ya kumlaumu kwa kuchukua mamlaka ya nchi kinyume cha Katiba.

Mara baada ya Jeshi la Zimbabwe kuonya kuwa litaingilia kati ikiwa chama tawala kitaendelea kufukuza wananchama wake ambao ni wapigania uhuru wa Taifa hilo, Chipanga alimlaumu Mkuu wa Majeshi kwa hali hiyo kwa kuiingiza nchi katika matatizo.

Mbele ya waandishi wa habari, Chipanga amesema yeye na umoja wa vijana kwa ujumla pamoja na wafuasi wote wa ZANU – PF, wako tayari kufa kumlinda Rais Robert Mugame na mkewe Grace Mugabe dhidi ya madhila kutoka katika jeshi hilo.

Chipanga alidai kuwa mapinduzi yaliyofanywa na jeshi hayana baraka kutoka katika jeshi lote la Zimbabwe hivyo hayana uhalali wowote wa kumuondoa Komredi Mugabe madarakani. Amesema lengo la Jenerali Costantine Chiwenga ni kufikisha ukomo wa utawala wa chama tawala cha ZANU – PF kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe.