Umasikini wachochea mimba utotoni

UMASIKINI wa kipato unachochea kuwapo kwa mimba za utotoni katika jamii. Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti alisema hayo katika warsha ya siku moja ya kutambulisha mradi na shirika hilo kwa wadau.

Mtengeti alisema utafiti uliofanywa na shirika hilo kwa kusaidiana na mashirika mengine, ulibaini umasikini wa familia husababisha familia zenye maisha magumu kupambana kwa bidii kutafuta chakula na mavazi ya watoto wao.

Alisema utafiti wa Demografia ya Afya Tanzania wa 2016 (TDHS) unaonesha asilimia 36 ya wasichana wa umri wa kati ya miaka 20-24 waliolewa kabla ya kufikia miaka 18. Mtengeti alisema, utafiti ulibaini asilimia 50 ya ndoa za utotoni inahusisha wanaume ambao ni wakubwa zaidi ya wanawake kwa miaka zaidi ya mitano hadi 14, hivyo kuoa wasichana wadogo na kusababisha wasichana kutokuwa na nguvu za kujadiliana na kunyanyaswa kingono.

“Ndoa za utotoni zinasababisha madhara mengi ya kuongezeka vifo vya akinamama na watoto, ugonjwa wa fistula kwa akinamama,” alieleza. Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Mpwapwa, Mery Chakupewa alisema kwa miaka mitatu iliyopita watoto 140 walikatisha masomo kwa ujauzito.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri aliyekuwa mgeni rasmi alisema, ni lazima wazazi na jamii nzima kurudi katika maadili kuokoa kizazi cha sasa na cha baadaye ili kuwa na taifa lisilo kuwa na wajinga wengi.

Alisema watu walioaminiwa katika malezi kama wazazi, walezi na walimu, wamegeuka na wamekuwa wakifanya mapenzi na wanafunzi. Shekimweri aliutaka uongozi wa wilaya kutafuta takwimu sahihi za matukio hayo ili kuisaidia wilaya kujua ukubwa wa tatizo hilo.