Kitila Mkumbo ajiunga ajiunga CCM

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Singida, Martha Mlata, ametangaza kuwa Profesa Kitila Mkumbo amejiunga CCM.

Aidha, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, amesema chama hicho kinatarajia kufanya vikao vya Uongozi vya Kitaifa vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam Novemba 19 hadi 23 mwaka huu, kujadili agenda mbalimbali hasa chaguzi.

Kupitia taarifa yake kwa umma jana, Mlata amesema, “Nafurahi kuwatangazia wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida na Tanzania kwa jumla kuwa, Ndugu, Profesa Kitila Mkumbo amejiunga tena na chama chetu... Ni fursa kwa mkoa kumpokea mwalimu baada ya kumpoteza mwanafunzi siku chache zilizopita.”

Kuhusu vikao vya CCM, Polepole alisema kupitia taarifa yake jana kuwa, vitapokea tathmini ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata 43 ambao kampeni zake zinaendelea.

Kadhalika, vitapokea, kuchuja, kutoa mapendekezo na kufanya uteuzi wa mwisho kwa walioomba dhamana ya uongozi katika ngazi za mikoa na taifa kwa CCM na jumuiya zake za Umoja wa Vijana, Umoja wa Wanawake pamoja na Jumuiya ya Wazazi.