Bunge laibana serikali wakala wa meli, yakubali

SERIKALI jana ilifanya mabadiliko ya jina katika muswada wa sheria uliofi kishwa wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (NASAC).

Kutokana na mabadiliko hayo muswada huo utabeba jina la Tanzania Shipping Agency Corporation (TASAC). Mabadiliko hayo yalifanyika baada ya kuzuka kwa ubishani mkubwa bungeni na kusababisha Spika wa Bunge, Job Ndugai kuahirisha bunge kwa saa moja na kuwapa nafasi serikali na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kujadiliana na kufikia muafaka wa jina hilo.

Kamati ya Bunge ya Miundombinu kupitia Mwenyekiti wake, Profesa Norman Sigalla alidai kamati yake inataka jina liwe Tanzania Maritime Authority ili kuendana na maudhui ya sheria inayotungwa kwani kazi yake kubwa ni kudhibiti.

Katika utetezi wake serikali kupitia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Mwanasheria mkuu wa Serikali, George Masaju wamedai serikali imeamua kutumia NASAC kwa sababu kazi ya shirika hilo ni kudhibiti na kufanya biashara ya uwakala wa meli.

Masaju alisema iwapo itabadilishwa jina hilo kuwa mamlaka au wakala itabidi kubadilishwe vitu vingi ndani ya sheria hiyo ikiwemo uandishi wa sheria hiyo ubadilishwe. Hata hivyo, Profesa Mbarawa alisema “serikali tumelichukua hili na tutalifanyia kazi kwani sheria hii si msahafu wala Biblia tunaweza hapo baadaye tukabadilisha jina lakini kwa leo tuipitishe”.

Kauli hiyo ilipingwa na Ndugai aliyetaka jina liendane na maudhui lakini akaonesha kuudhika na jina hilo linalofanana na NASACO ambayo ilikuwa na sifa mbaya ya rushwa. Ndipo akaahirisha bunge hilo kwa saa moja kutoka saa 12:30 jioni hadi saa 1:30 usiku ili serikali na kamati ya miundombinu wajadiline na kuja na makubalino.

Awali Serikali ilisema kwa kuanzisha Shirika hilo, sasa wakala binafsi wa meli hawataruhusiwa kuhusika na uondoshaji wa shehena za madini, makinikia, wanyama hai na nyara za serikali.

Pia wakala hao binafsi wa meli hawataruhusiwa kupokea nyaraka za shehena kutoka kwa wenye meli, uhakiki wa shehena inayoingia na kutoka bandari za Tanzania Bara, uondoshaji shehena zitokanazo na bidhaa za madini, petroli, silaha.

Kazi hizo zote zitafanywa na TASAC. Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamepinga shirika hilo kufanya biashara na kudhibiti wakala za meli kwa madai zitaleta mgongano wa kimaslahi.

Akiwasilisha Muswada wa Sheria wa Shirika la Uwakala la Meli Tanzania (TASAC) wa Mwaka 2017, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema wakala binafsi akishindwa kutekeleza majukumu yake ama kwa kufilisika au kupoteza sifa za kumiliki leseni, shirika hilo litatekeleza kazi za wakala huyo ili kuziba mwanya kwa lengo la kuhakikisha huduma zinaendelea hadi mwenye meli atakapoteua wakala mwingine.

Alitaja mamlaka ya shirika hilo ni kufanya ukaguzi wa meli za kigeni na udhibiti meli zilizosajiliwa Tanzania, udhibiti wa vivuko vya kibiashara, kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji, kudhibiti kuratibu na kulinda mazingira ya bahari za Tanzania Bara.

Profesa Mbarawa alisema kampuni ya uwakala wa meli itatakiwa kumilikiwa na Watanzania kwa kiwango cha hisa kisichopungua asilimia 60 ya hisa za kampuni husika. Wakati waziri akibainisha hayo, wabunge kupitia Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, wapinzani na wengine waliochangia, walipinga shirika hilo kufanya shughuli za udhibiti na biashara ya uwakala wa meli kwa madai kutaleta mgongano wa maslahi na kusababisha wafanyabiashara wakubwa kukimbia na kuzuia ushindani wa kibiashara.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, Moshi Kakoso ameishauri serikali kutenganisha masuala ya udhibiti na ufanyaji wa biashara ili kuondoa mgongano wa kimaslahi kwa mdhibiti kufanya kazi za uwakala.

Alisema kitendo cha mwenye meli kutopewa leseni ya uondoshaji wa shehena ni ngumu katika dunia ya sasa katika kuepuka muingiliano huo na kufafanua “jambo la msingi ni kuwa na udhibiti na ufuatiliaji wa karibu ili kuepuka ubadhirifu ambao awali ulikuwa unajitokeza.”

Msemaji wa kambi ya upinzani, Suzan Lyimo alishauri serikali kutunga miswada miwili tofauti itakayowezesha kuwa na mamlaka ya udhibiti wa wakala wa meli na usafiri wa njia ya majini na muswada mpya utakaowezesha kuwa na shirika lenye kutoa huduma za uwakala wa meli kama wakala.

“Hakuna anayepinga serikali kufanya biashara bali ni muhimu serikali ifanye biashara zake bila kuongeza ukiritimba katika kukuza sekta hii yenye umuhimu kwa uchumi wa nchi,” alisema na kuongeza:

Haiwezekani shirika hilo likawa mwamuzi wa mpira na mchezaji wa mpira wakati mmoja na hata katika udhibiti na utendaji wake ni lazima mgongano mkubwa wa kimaslahi utokee na kukwamisha sekta hii kubwa.”