Wabunge watuhumu TRA kuwa ndiyo ‘wezi’ Bandarini

WABUNGE wamewanyooshea kidole wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaokagua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kuwa ni wezi na wanaipotezea mapato serikali hivyo wadhibitiwe.

Walitoa tuhuma hizo jana wakati wakichangia Muswada wa Sheria ya Kuanzishwa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (NASAC) uliowasilishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa bungeni mjini Dodoma jana.

Wabunge hao walisema watumishi wa TRA pekee ndiyo wanaohusika na ukaguzi wa mizigo bandarini na wamehusika kwenye ufisadi mwingi wakishirikiana na wafanyabiashara wakubwa na serikali inawafahamu wote lakini haijawachukulia hatua.

Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kassim Ahmed (CUF) alisema “TRA ndiyo inayofanya wizi bandarini wa fedha na mizigo, tunataka mtueleze Nasac itawadhibiti vipi, Sumatra na TPA wako safi na hawajui ndani mzigo ukoje, imewahi kutokea Mkurugenzi wa Sumatra akatuambia aliidhinisha kontena sita zisafirishwe akiambiwa zina majani ya chai kumbe ndani kulikuwa na bangi na yeye hawezi kujua kilichomo ndani, lakini TRA wanajua.”

Alilaumu watendaji wa TRA kuhusika kwenye ufisadi kwa kutoza ushuru mkubwa wafanyabiashara wadogo na kuwalipisha kodi ndogo wafanyabiashara wakubwa hali inayosababisha wafanyabiashara wadogo wengi kufa kibiashara.

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) alisema kwenye Bandari ya Dar es Salaam kunafanyika ufisadi mkubwa kwa watumishi wa TRA kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa na kusisitiza “Muswada umeletwa kwa sababu ya udhibiti ufisadi, lakini hata waziri anawajua mafisadi wakubwa bandarini na siyo suala la Masamaki (mtumishi wa TRA) wa pekee, Home Shopping Centre bado wanapiga dili, lakini hawa hawashughulikiwi.”

Naye Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM) alisema iwapo hakutakuwepo nia ya kuwadhibiti watumishi wa TRA wanaokagua mizigo na kufanya wizi na kuitia hasara serikali, sheria hiyo ya kuanzishwa Nasac haitasaidia.

“Kufungwe kamera za CCTV kila eneo kudhibiti watendaji wezi kwani mfano tumeona kwenye ufungaji almasi watendaji wanakuwepo wanne hadi sita lakini wote wanabariki wizi, sehemu nyingi serikali inategmea mageti ambapo wasimamizi wake nao ni wezi,” alisema Mwakasaka