Puuzeni kauli ya Lowassa kuhusu katiba -UVCCM

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umewataka Watanzania kuyapuuza madai ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ya kumtaka Rais John Magufuli aruhusu mjadala wa Katiba mpya ili kuachana na vita ya uchumi, mapambano dhidi ya rushwa na ufi sadi.

Pia umoja huo umedai kuwa yanayotaka kufanywa na Lowassa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ni dhamira ovu ya kuamsha vurugu na ghasia ili kuiondoa serikali katika mstari, mikakati na mipango ya kutumikia wananchi na kuwaletea maendeleo ya kisekta.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Upanga jiijini Dar es Salaam kutokana na matamshi ya Lowassa aliyoyatoa Arusha kwenye mkutano wa kampeni za udiwani sanjari na Mwenyekiti waTaifa wa Chadema, Freeman Mbowe aliyezungumza akiwa Mtwara.

Shaka alisema kinachotamkwa na Lowassa ni mkakati wa majaribu hatari ili kuitia nchi kwenye machafuko, ghasia na fujo kwa nia ya kuitoa serikali kwenye mwelekeo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015/2020.

Alisema Chadema kina majuto kutokana na maamuzi hasi ya kuwakaribisha mafisadi na kujikuta kikipoteza ajenda yake kwa wananchi hivyo wanataka kupita mlango wa madai ya Katiba jambo ambalo halimo kwenye Ilani iliyokipa ridhaa na ushindi CCM.

“Tunawapa indha na tahadhari wananchi wasikubali kufuata mkumbo wa siasa za kibabe za Lowassa, Mbowe na Chadema kudai Katiba Mpya kibabe. Katiba iliyopo ni ya kidemokrasia iliyoliongoza Taifa kwa miaka 54 ya Uhuru na Muungano,” alieleza Shaka.