Bunge launda kamati kuchunguza gesi, uvuvi

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameunda kamati za kushughulikia sekta ya gesi na ya uvuvi wa bahari kuu ili kufahamu kwa nini hazichangii pato la taifa.

Ndugai alimrudisha tena mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko kuwa mwenyekiti wa kamati ya gesi ambapo aliwahi kuwa kwenye kamati iliyochunguza ya madini kwa ajili ya kubaini dosari zilizomo katika sera na sheria zake na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu akipelekwa sekta ya uvuvi.

Akitangaza jana Spika alisema anatumia kanuni ya 5 (1) ya kanuni za Bunge toleo la 2016 ambayo inampa madaraka ya kuunda kamati kwa kadri atakavyoona inafaa. Alisema kumekuwa na hali ya kusuasua kwa sekta hizo ambapo uvuvi wa bahari kuu unachangia pato la taifa kwa asilimia 1.4 ambayo ni sawa na Sh bilioni 3.2 wakati kuna zaidi ya Sh bilioni 400 ambazo zinapotea bure.

Alisema ukubwa wa ukanda wa bahari katika uvuvi wa Tanzania unalingana na Namibia ambayo inaingiza pato kwa asilimia 10, hivyo kuna kila sababu ya kupitia upya sekta hiyo ikiwemo kuangalia mirahaba ya leseni za uvuvi wa meli zinazovua bahari kuu.

Wajumbe wa kamati ya uvuvi ni Zungu, Salum Mwinyi Rehani, Masoud Salim Abdala, Tauhida Nyimbo na Mbaraka Dau. Wengine katika kamati hiyo ni Dk Immaculate Semesi, Dk Christina Ishengoma, Stanslaus Mabula, Mussa Mbarouk na Cosato Chuma ambao wataongozwa na Mwenyekiti wao Anastazia Wambura.

Kamati ya sekta ya gesi itakuwa chini ya wajumbe Innocent Bashungwa, Dunstan Kitandula, Dk Seleman Yusufu, Wanu Hafidhi Ameir, Oscar Mukasa na Ruth Molell. Wajumbe wengine katika kamati hiyo ambayo iko chini ya uenyekiti wa Biteko ni Richard Mbogo, Omari Kigua, Abdallah Mtolea na Sebastian Kapufi.

Ndugai alimwagiza Katibu wa Bunge kuangalia namna ya kuwawezesha wabunge hao ili waanze kazi na kamati zao zimetakiwa kufanya kazi ndani ya siku 30 tangu siku watakayokabidhiwa majukumu yao.

Sambamba na kuunda kamati, Ndugai amesema atawachongea Mawaziri kama watashindwa kupeleka bungeni sheria inayotambua Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi. “Mmetupiga danadana sana, hivi ni nani aliyekalia Muswada huo ama mnataka siku moja niamue kwenda Dar es Salaam tena, nasema kama bado nimekalia kiti hiki hakuna mtu ataweza kupenyeza ajenda hiyo,” alisema.

Kiongozi huyo alisema mawaziri wamekuwa wakilidanganya Bunge kila wakati kuwa Muswada huo unapelekwa bungeni lakini kila wakati Bunge linamaliza mkutano hakuna kitu kama hicho licha ya kuwa hata tamko la Makao Makuu ya Dodoma ni la Rais John Magufuli mwenyewe.

Alimwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa akishindwa kupeleka Muswada huo katika mkutano wa 10 wa Bunge la 11 angalau kusomwa kwa mara ya kwanza, basi atamwambia Rais nini kinachoendelea.