Rais Mugabe aonekana hadharani shangwe zalipuka

KWA mara ya kwanza baada ya kuzuiliwa na jeshi nyumbani kwake, Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe (93), ameonekana hadharani, akihudhuria sherehe za mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Harare.

Mashuhuda wa tukio hilo wanasema Rais Mugabe ambaye ameshikilia msimamo wake wa kutojiuzulu hadi amalize kipindi chake cha urais mwakani, alishangiliwa kwa nguvu na wananchi wakati akihutubia mahafali hayo.

Tangu Jumatano iliyopita Rais Mugabe alikuwa chini ya kizuizi cha jeshi la nchi hiyo nyumbani kwake nje kidogo ya mji wa Harare. Rais Mugabe aliendelea kushikilia msimamo wake wa kutojiuzulu wadhifa wake, wakati wa mkutano kati yake na majenerali wa ngazi ya juu wa kijeshi ambao walichukua udhibiti wa Zimbabwe.

Mazungumzo hayo yalifanyika mjini Harare, baada ya wanajeshi kuzuia barabara kuu, kudhibiti Kituo cha Televisheni ya Taifa na kumweka katika kizuizi cha nyumbani Mugabe na mkewe Grace na mawaziri kadhaa.

Kituo hicho cha televisheni kilimuonesha Mugabe akiwa amevalia koti la rangi ya bluu na suruali ya kijivu akiwa amesimama na Mkuu wa Majeshi, Constantino Chiwenga aliyekuwa amevalia sare za kijeshi.

Umoja wa Afrika, SADC walaani mapinduzi Awali, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma aliliambia Bunge la nchi yake mjini Cape Town, kwamba ni mapema mno kuchukua uamuzi thabiti kutokana na hali ya kisiasa iliyopo, ambayo muda si mrefu itajulikana wazi.

Umoja wa Afrika (AU) umesema utairuhusu Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuwa mpatanishi katika mzozo huo wa kisiasa wa Zimbabwe. Kamishna wa Amani na Usalama wa AU, Smail Chergui alisema jana kuwa umoja huo una matumaini kwamba hatua ya jeshi la Zimbabwe kuchukua madaraka, inaonesha kuwa kuna juhudi za kufuata sheria, badala ya kuwepo mapinduzi.

Alisema kuwa wajumbe wa SADC wamefanikiwa kukutana na Rais Mugabe na kwamba Afrika ina imani na juhudi zao. Kwa upande wake Mwenyekiti wa AU, Alpha Conde alisema umoja huo hautaruhusu mapinduzi ya kijeshi nchini Zimbabwe.

Akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari, Conde ambaye ni Rais wa Guinea, alitoa mwito wa kurudishwa haraka kwa utawala unaotambuliwa kikatiba na alitaka Katiba ya Zimbabwe iheshimiwe.

UN yasisitiza diplomasia Jumuia ya Kimataifa pia imekuwa ikiufuatilia mzozo huo kwa karibu ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) , Antonio Guterres ametoa mwito wa kupatikana suluhu kwa njia ya amani nchini humo.

Msemaji wa Katibu Mkuu huyo wa UN, Stephane Dujarric alisema umoja huo una wasiwasi na kwamba hautaki kuona nchi hiyo inakosa utulivu. Katika taarifa yake, Guterres alisema anafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea nchini Zimbabwe, na alitoa mwito wa kuwepo utulivu na kusisitiza umuhimu wa kupatikana suluhisho kwa njia ya amani, ikiwemo kufanya mazungumzo.

Katibu huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliunga mkono juhudi zinazofanywa na SADC katika kuumaliza mzozo huo, akisema ndio njia sahihi zinazokubalika katika kumaliza mzozo huo.

Ujerumani yamfagilia Mugabe Naye msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Rainer Breul alisema Ujerumani na washirika wake wa Umoja wa Ulaya wamewasihi viongozi wa jeshi nchini Zimbabwe kuepusha ghasia kutokana na hali iliyopo nchini humo.

Ujerumani imezitaka pande zote kushirikiana ili kupata ufumbuzi kwa amani huku ikisisitiza kuwa njia sahihi ni kuheshimu Katiba kwa kutambua utawala wa kidemokrasia wa Rais Mugabe ili umalize muda wake rasmi.

Kwa miaka mingi, Ujerumani na Zimbabwe zimekuwa na uhusiano mzuri na imara. Mwaka 1982 aliyekuwa Kansela, Helmut Schmidt alimpongeza Mugabe, ambaye kwa wakati huo alikuwa Waziri Mkuu, kwa kusaidia katika harakati za ukombozi na kuchangia kwa kiasi kikubwa nchi hiyo kujipatia uhuru wake kwa njia ya amani