Rais Mugabe wa Zimbabwe hatimaye ang’oka

RAIS Robert Mugabe wa Zimbabwe aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 37, hatimaye amejiuzulu. Amefanya hivyo baada ya shinikizo la kuachia madaraka lililodumu kwa zaidi ya wiki moja.

Spika wa Bunge la nchi hiyo, Jacob Mudenda alisema jana jioni kuwa barua kutoka kwa Mugabe, ilieleza kwamba uamuzi huo aliouchukua ni wa hiari na kwamba amefanya hivyo ili kuruhusu kukabidhi madaraka pasipo vurugu. Uamuzi huo wa Mugabe umekuja baada ya Jeshi kuchukua udhibiti wa nchi na yeye kuondolewa kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama chake tawala cha Zanu-PF.

Tangazo hilo liliwashitua wengi na pia lilisitisha hatua ya bunge la nchi hiyo kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Mugabe, baada ya hatua za kumwomba ajiuzulu kukataliwa moja kwa moja na kiongozi huyo. Wabunge wa nchi hiyo walionekana kurukaruka kwa furaha kwa uamuzi huo wa Mugabe na kufanya watu kuingia mitaani kuanza kusherehekea.

Hapo awali Mugabe alikataa kujiuzulu, licha ya shinikizo lililofanywa na jeshi la nchi hiyo kutaka kuchukua madaraka na maandamano yaliyomtaka ajiuzulu nafasi hiyo kwa hiari yake. Mugabe amekuwa madarakani tangu mwaka 1980.

Ilielezwa kuwa chanzo kilichotajwa hapo awali, kilichosababisha haya yote ni kitendo cha Mugabe kumfukuza kazi aliyekuwa Makamu wake wa Rais, Emmerson Mnangagwa, ambacho hakikuungwa mkono nchini humo, kwa kuwa kulikuwa na dalili za kutaka mke wake, Grace Mugabe kuja kurithi kiti cha urais.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini humo, Rais Mugabe aliwekwa kizuizini nyumbani kwake baada ya Jeshi kuchukua udhibiti wa nchi na haikujulikana wa api hasa alipo mke wake. Wananchi wa Zimbabwe walianza kupoteza uvumilivu baada ya Mugabe kuendelea kung’ang’ania madarakani, licha ya kutakiwa kujiuzulu haraka.

Mapema juzi wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zimbabwe, walikifunga chuo hicho wakishinikiza Mugabe aondolewe madarakani. Wanafunzi hao waliokusanyika kwa wingi kwenye eneo la wazi chuoni hapo na kuanza kuhamasishana, walibeba mabango yaliyoandikwa ujumbe wa kumpinga Mugabe. Baada ya kuhamasishana, ilipofika saa nne asubuhi, wanafunzi hao walianza kuziba njia na wengine waligomea kufanya mitihani yao ya mwisho wa mwaka.