Vituo vya matibabu ya bure vyaongezwa

KUTOKANA na idadi kubwa ya wananchi kujitokeza katika upimaji wa afya bure ndani ya meli maalumu kutoka China, wamelazimika kuongeza idadi ya vituo na kupunguza muda wa mapumziko ili kuhakikisha kila mwananchi aliyepewa namba anapata huduma.

Aidha, mpaka sasa zaidi ya wagonjwa 17 wamefanyiwa upasuaji mkubwa, kitendo ambacho kimesaidia kupunguza gharama za matibabu, ikiwemo kusafirisha wagonjwa nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao chake na Kiongozi wa meli hiyo, Mkuu wa Mkoa Paul Makonda alisema wameamua kuweka vituo katika eneo la Trafiki makao makuu na eneo jirani na ilipo meli hiyo ili wagonjwa wenye magonjwa ya kawaida waweze kuhudumiwa katika vituo hivyo na kutoa fursa kwa wenye magonjwa makubwa, waweze kupatiwa huduma ndani ya meli hiyo.

Aidha, alisema madaktari wa China wameridhia kuongeza muda wa kutoa huduma kwa kupunguza muda wa mapumziko kutoka saa mbili hadi saa moja na kutoa matibabu usiku na mchana.

“Nawashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kutokana na wingi huo hatuwezi kuwarudisha nyumbani tunahangaika ili waweze kupata huduma kwa sababu mgonjwa aliyekuja kupata huduma hawezi akarudi na ugonjwa wake na niwaambie tu msimamo wa madaktari hawa kuondoka baada ya siku tano za huduma uko palepale na hakuna muda utakaoongezwa,” alisema Makonda.

Hata hivyo, wananchi ambao bado wanaendelea kujitokeza, wamemuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia ili waweze kupata huduma katika senta zilizowekwa katika hospitali za Amana, Mwananyamala, Temeke na Muhimbili ili waweze kupatiwa huduma kwa kuwa watu wengi wanakwenda katika hospitali hizo lakini hawapatiwi huduma.

“Mimi nimekwenda Amana baada ya kusikia kuwa kuna madaktari wa China wanatoa huduma kule, lakini nikaambiwa niende ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupata maelekezo, sasa sijajua kwa nini imekuwa hivyo na nimekuja huku bandarini wananiambia namba hazitolewi kwa sasa tunaomba watusaidie,” alisema Yusta Ndumbikwa.

Licha ya Makonda kusema kuwa muda hautaongeza wananchi wameendelea kuomba muda uongezwe, kwa kuwa bado watu wanaohitaji huduma wapo wengi na muda ni mchache.

“Mpaka sasa sijapata namba na sijui kama nitapata, naomba watusaidie jamani hatuna fedha za kwenda hospitali za kulipia, tunaomba watusaidie,” alisema Hamza Kitunda, mkazi wa Mbagala Kuu.