TSN yaomba mahusiano zaidi na umma

TAASISI ya magazeti ya Serekali yaani TSN imetoa rai kwa Taasisi za Umma na Binafsi pamoja na Serekali za Mitaa Nchini kukuza mahusiano ya kiutendaji zaidi.

TSN ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Dailynews, Sundaynews, Habarileo, Habarileo Jumapili na Sport Leo ni moja wa taasisi zilizodhamini semina ya siku tatu iliyoandaliwa na Chama cha Wahasibu nchini yaani TAA kwa watendaji wakuu wa Serekali za Mitaa inayofanyika Dodoma.

Afisa Masoko Mwandamizi wa TSN Mr Goodluck Chuwa ameeleza hilo leo mjini Dodoma wakati akiwasilisha mada ya TSN juu ya jukumu lake kwa umma la kuhabarisha na kufanya machapisho mbalimbali ya serekali na ya binafsi.

Ameziomba taasisi zote za umma na binafsi, kuwa na mahusiano ya kibiashara na kushauri wajumbe wa semina hiyo kwamba "ni vizuri kukuza mahusiano ya kikazi baina yetu TSN na taasisi zote kwa pamoja ili kufanikisha lengo la Serekali kufikia azma ya maendeleo ya watu na jamii kwa haraka zaidi kwa kutumia rasilimali chache zilizopo" ameeleza Mr Chuwa.

Ameongeza kwa kusema kwamba, TSN imeboresha zaidi utendaji wake wa ndani ikiwamo kuzingatia uharaka katika kutoa huduma za kihabari na matangazo pia. Pia Mr Chuwa ameeleza TSN inaelekeza nguvu zaidi katika teknologia ya kisasa ya mawasiliano akiwamo mitandao ya kijamii mfano facebook, twitter na Intagram na zinginezo lengo likiwa ni kuharakisha utoaji huduma na taarifa ili kuwafikia walengwa kwa haraka zaidi.

Kuhusu suala la Ubunifu, Mr Chuwa amesema, TSN imeanzisha kwa kuwekeza kwenye mtambo wa kisasa wa uchapaji yaani "Commercial Printing" na kufafanua zaidi kwamba lengo ni kuweza kutoa huduma za uchapati zenye viwango vinavyohitajika sokoni.

Chuwa alijikita zaidi katika uchapishaji wa kisasa ambapo ameziomba wazi wazi taasisi za SSRA, LAPF, PPF, PSPF, GPF, WCF, NSSF, TCRA, TRA, CRDB, TTCL na zingine alizotaja kwa wingi ili waje TSN kufanya makubaliano ya kibiashara kuhusu uchapaji wa kisasa kwa gharama nafuu zaidi lakini kwa ubora.

Kwa kumalizia Mr Chuwa alitaja jukumu la nne la TSN kwa sasa ambalo ni "Uwajibikaji". Amesema TSN katika hili, imedhamiria kulitumia soko la Afrika Mashariki kupenyeza huduma zake kwa kupitia machapisho yake na pia kukuza lugha ya Kiswahili kwa majirani zetu.

Alifafanua zaidi kwamba "kwa sasa TSN imeshaanza kujitanua zaidi na imefika hadi nje ya mipaka ya nchi hadi Kigali Rwanda, Kampala Uganga, Nairobi Kenya" na kwingineko katika jumuiya yetu na kutoa rai kwamba, "wadau wa nje wasije kutupita kutumia huduma za TSN na kuacha nyuma sisi wa nyumbani" hivyo akatoa rai kukuza mahusiano zaidi.

TSN ni moja wa wawezeshaji wa hii semina ya siku tatu kwa ajili ya kuwapatia washiriki uelewa zaidi kwa watendaji wakuu wa Serekali za mitaa ili watumie kwa tija zaidi rasilimali fedha za umma kwa manufaa zaidi.

TSN imekuwa na mahusiano mazuri ya kikazi na Serekali zote za Mitaa nchini kupitia ALAT pia Takribani taasisi zote za umma ambapo machapisho mbalimbali ya umma mfano Sabine, taarifa za mahesabu na makala mbalimbali zimekuwa zikichapishwa na magazeti ya TSN.