Wakulima, wanunuzi pamba waonywa

WAKULIMA wa pamba wametakiwa kuvuna pamba yao mapema ili kuepusha zao hilo kupoteza ubora.

Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba aliyasema hayo jana mjini Uyui alipokwenda kuangalia maandalizi ya kilimo cha zao hilo na kampeni za uhamasishaji wananchi kulima kwa wingi zao hilo zinazoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.

Alisema pamba haina budi kuvunwa mapema, badala ya kusubiri mimea yote shambani ichanue kwa kuwa hali hiyo husababisha pamba iliyotangulia kukamaa, kupata vumbi na uchafu mwingine na hivyo kupungua ubora.

Naye Mwanri aliwaonya wakulima wenye tabia ya kuchanganya pamba na uchafu wakati wa uuzaji wa zao hilo kuacha mara moja vinginevyo, watachukuliwa hatua za kisheria. Alisema kazi ya kuwakamata itawahusu pia wakulima watakaochanganya pamba na mazao mengine na wanunuzi watakaochezea mizani ili kuwaibia wakulima.