CCM yawafunda madiwani wake wapya Hai

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Hai, Kilimanjaro Kumotola Kumotola amewataka madiwani wateule wawajibike na kutimiza ahadi zao bila kujali itikadi za vyama.

Kumotola alisema hayo baada ya Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo hilo, Yohana Sinto, kuwakabidhi madiwani watatu (CCM) vyeti vya ushindi baada ya kushinda katika uchaguzi mdogo Jumapili iliyopita.

Alisema chama hakitawavumilia madiwani watakaoshindwa kuitisha vikao vya kikatiba na kufanya mikutano kwa wananchi kwani kuitisha mikutano kunasaidia kutambua na kutatua changamoto zilizopo.

Diwani Mteule wa Kata ya Weruweru, Salehe Msingesi alisema atahakikisha anatimiza ahadi alizozitoa kwenye mikutano yake ya kampeni ikiwemo kutatua kero ya ubovu wa miundombinu ya barabara.

Diwani mteule wa Kata ya Mnadani, Nasibu Mndeme na wa kata ya Machame Magharibi, Martini Munisi, walisema watashirikiana na Halmashauri na chama kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi.

CCM imeshinda kata zote tatu katika uchaguzi huo mdogo na hivyo Baraza la Madiwani Hai litakuwa na mchanganyiko wa madiwani 14 wa kuchaguliwa Chadema na CCM madiwani watatu wa kuchaguliwa.