CUF yamtakia safari njema ya kisiasa mbunge wake Mtulia

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeridhia kitendo cha kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia na kumtakia safari njema ya kisiasa.

Naibu Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho, Mbarala Maharagande katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, alisema kitendo cha Mtulia kujiuzulu ubunge, uanachama na nyadhifa zake nyingine ndani ya chama hicho, ni haki yake kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na ya nchi kwa ujumla.

“CUF ilipokea kupitia mitandao ya kijamii taarifa ya kujiuzulu nafasi zake zote katika chama chetu, na tumemsikia akieleza sababu zake za kufanya maamuzi hayo, ingawa sababu alizozitoa CUF haikubaliani nazo,” alisisitiza Maharagande.

Alisema chama hicho, kilitarajia hali hiyo tangu mapema na wala haikushtushwa na maamuzi yake kutokana na taarifa za kiintelijensia. “Tunatoa pole kwa Wana- CUF na wananchi wa Jimbo la Kinondoni ambao walipambana kwa hali na mali kuhakikisha kuwa mabadiliko ya kisiasa nchini yanapatika kwa kusimamia ushindi wa chama hicho na mbunge katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2015,” alisema.

Alieleza kuwa chama hicho, kinamtakia Mtulia safari njema ya kisiasa huko alikokwenda, ni haki na uhuru wake ambao unapaswa kuheshimiwa na kila mwanachama wa CUF. Juzi Mtulia, alitangaza kujiuzulu rasmi uanachama na ubunge kupitia chama hicho cha CUF na kujiunga na CCM ili kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kupambana na mafisadi na kuliletea maendeleo taifa.

Katika maelezo yake ya kujiuzulu, alifafanua kuwa amefikia uamuzi huo kwa kuwa mambo yote waliyoahidi akiwa upinzani tayari yanafanywa vizuri zaidi na CCM hivyo ni vigumu kuwa mpinzani