Polisi yaanza upelelezi mkali uvamizi kwa Mbunge Nassari

JESHI la Polisi mkoani Arusha limesema kuwa linafanya uchunguzi wa tukio la kuvamiwa kwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari.

Nassari alivamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake Meru Nkwaninkole na mbwa wake kupigwa risasi katika shambulio la silaha lililofanywa usiku wa kuamkia juzi na watuhumiwa kutimkia kusikojulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alikiri kupata taarifa ya tukio hilo na kusema kuwa kazi ya uchunguzi iachiwe jeshi hilo. Nassari alisema mbele ya waandishi wa habari kuwa alivamiwa na watu hao saa sita usiku baada ya kutoka kuhudhuria kongamano la vijana lililokuwa likifanyika katika Chuo cha Mafunzo na Maendeleo ya Kimataifa (MST DC) eneo la Denish.

Kwa mujibu wa Nassari akiwa ndani kwake amelala ghafla alisikia kelele za mbwa akibweka na alipojaribu kuchungulia alisikia mlio wa risasi na ndipo alipochukua bunduki yake na kuanza kufyatua juu kwa lengo la kujihami.

Hata hivyo, hakufahamu idadi kamili ya wahalifu hao kwani wakati alipotoka nje wahalifu hao tayari walikuwa wameshatoweka eneo hilo kwa kuruka ukuta baada ya kusikia akijibu mapigo kwa kutumia silaha yake ya kujilinda anayoimiliki.