AU yataka Afrika yote isiwe na viza

TUME ya Umoja wa Afrika (AU) imesema uamuzi wa Serikali ya Kenya, kuruhusu Waafrika wote kwenda nchini humo bila viza ni wa kihistoria. Imetoa mwito kwa nchi nyingine za Afrika, ambazo hazijafanya hivyo, kuiga mfano huo ili kuboresha matembezi ya wananchi barani humo.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Moussa Faki Mahamat ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa amefurahishwa na tangazo la Rais Uhuru Kenyatta la kuruhusu Waafrika wanaokwenda Kenya, wapewe viza wanapofika nchini humo.

Alimpongeza Kenyatta kwa uamuzi huo na kutoa mwito kwa nchi nyingine, kuruhusu Waafrika wawe huru ndani ya bara hilo. Kwa mujibu wa Rais Kenyatta, uamuzi huo utakuza biashara na usalama, utaongeza ushirikiano na kupunguza siasa za chuki ndani ya bara hilo.

Kenya imeungana na Rwanda, Mauritius na Shelisheli ili kuruhusu Waafrika kuingia kwenye nchi hizo bila viza. Kuanzia mwaka jana, Ghana iliweka utaratibu wa kutoa viza mara wananchi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wanapofika nchini humo.

“Leo naagiza kwamba, Mwafrika yeyote anayependa kutembelea Kenya atakuwa na uwezo wa kupewa viza eneo anapoingilia... kadiri tutakavyokuwa huru kusafiri na kuishi pamoja ndipo tutakavyotengamana zaidi na kunufaishwa na tofauti zetu,” alisema Rais Kenyatta baada ya kuapishwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Moi-Kasarani jijini Nairobi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri Kenya (FKE), Jacqueline Mugo alisema licha ya kurahisisha matembezi ya wananchi, kutolewa kwa viza baada ya mtu kufika nchini humo kutaokoa muda na kupunguza gharama.

“Hili ni jambo zuri na kama ambavyo tumekuwa tukiomba ili kuiwezesha Afrika ijioneshe duniani kuwa ni soko moja,” alisema Mugo. Mwenyekiti wa Chama Cha Wazalishaji Kenya (KAM), Flora Mutahi alisema kufunguliwa kwa mipaka ya Kenya ni hatua nzuri katika kuongeza mvuto wa nchi hiyo kwa wawekezaji.

Mkurugenzi wa Uhamiaji nchini Kenya, Gordon Kihalangwa alisema hadi linatolewa agizo hilo mambo mengi yamezingatiwa, lakini pia linahitaji kuangaliwa kwa makini ili kupata namna bora ya kulitekeleza. Alisema, ingawa watu wameruhusiwa kwenda Kenya bila viza, wageni watachunguzwa ili kuepuka wenye lengo baya.

Hivi karibuni, Rwanda ilitangaza kuruhusu watu kutoka nchi yoyote duniani kwenda nchini humo bila viza, na kwamba watapewa kwenye sehemu watakazoingilia. Balozi wa Rwanda nchini Kenya, James Kimonyo alitoa mwito kwa nchi nyingine za Afrika, kuruhusu watu kuingia huko bila viza ili kujenga mazingira ya mtangamano wa bara la Afrika.

Kwa mujibu wa Kimonyo, uamuzi huo una manufaa kwenye biashara na uwekezaji. Umoja wa Afrika (AU) upo kwenye mchakato, kuwezesha wananchi kutoka nchi yoyote barani humo kuwa huru kwenda popote ndani ya bara hilo.

Rwanda imetangaza kuwa, kuanzia Januari Mosi mwakani, raia wa nchi zote duniani watakaokwenda nchini humo na kukaa wa siku chache, hawatapaswa kuomba viza kabla. Wananchi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za Burundi, Kenya, Uganda, Tanzania na Sudan Kusini, watatakiwa kuonesha vitambulisho baada ya kuwasili Rwanda.

Rais Kenyatta alisema, wananchi wote kutoka nchi wananchama EAC watakapokwenda Kenya, watahudumiwa kama Wakenya. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mwananchi kutoka ndani ya EAC atayekwenda Kenya, atapaswa kuwa na kitambulisho tu kitachomwezesha kufanya kazi, kufanya biashara, au kumiliki ardhi nchini humo.

Kwa mujibu wa tangazo la Serikali ya Rwanda, baada raia wa nchi zote duniani kuwasili nchini humo kwa njia yoyote, Rwanda itawapa viza ya siku 30. Kwa kuzingatia tangazo hilo, raia kutoka nchi wanachama wa Soko la Pamoja la Nchi za Kusini na Mashariki ya Afrika (COMESA), hawatahitajika kuomba viza ya chini ya siku 90.

Baada ya kuwasili Rwanda, watapewa viza watakayoilipia kiwango kilichowekwa kwa kuzingatia Itifaki ya COMESA ya uhuru wa wananchi kwenda popote, kufanya kazi popote, kutoa huduma nchi yoyote, haki ya kujiendeleza na kuishi popote.

Kwa sasa raia kutoka nchi wanachama wa COMESA wakifika Rwanda wanapewa visa ya siku 30 kama ilivyo kwa watu wengine wenye hati za kusafiria za Afrika. Kwa mujibu wa tangazo la Kurugenzi Kuu ya Uhamiaji, kuanzia Novemba 16 mwaka huu imeingia mkataba wa kuondoa viza kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na huduma, kwa nchi za Djibouti, Ethiopia, Gabon, Guinea, India, Israel, Morocco na Uturuki.

Kwa mujibu tangazo hilo raia wa nchi 18 wanaopenda kutembelea Rwanda hawatahitajika kuomba au kulipia visa. Kwa nchi hizo, wananchi wake wakifika Rwanda watapewa visa bila kulipia.

Wananchi hao watapaswa kuonesha nyaraka halali za safari, wakiwemo watakaopaswa kuonesha kitambulisho cha taifa na wengine hati halali ya kusafiria. Wananchi hao ni wenye hati za kusafiria kutoka nchi za Benin, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Ghana, Guinea, Indonesia, Haiti, Senegal, Shelisheli, Sao Tome and Principe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mauritius, Ufilipino na Singapore.

Serikali ya Rwanda imetangaza kuwa, Wanyarwanda wanaoishi nje ya nchi hiyo wenye uraia wa nchi mbili, kuanzia sasa wataruhusiwa kuingia nchini humo kwa kuonesha vitambulisho vya taifa.

Awali, watu pekee waliopewa viza bure baada ya kuwasili nchini humo ni Wanyarwanda waliosafiri kwa hati za kusafiria za nje na wenye hati za halali za kusafiria za Rwanda. Kwa mujibu wa tangazo la serikali, raia wa nje wanaoishi Rwanda wataanza kutumia vitambulisho vyao vya ukaazi kuingia nchini humo na kama wana vibali halali vya kuishi huko wataweza pia kutumia milango ya kielektroniki kupita kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali.