Israel yataka nafasi Umoja wa Afrika

WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema, nchi hiyo inakuza uwepo wake na kuzidisha uhusiano na Afrika kwa kuwa ina imani na hali ya baadaye ya bara hilo na inalipenda.

Alisema angetamani kupata nafasi hata ya kuwa mwangalizi ndani ya Umoja wa Afrika (AU) akisisitiza kuwa Israel inaweza kuboresha maisha ya watu popote, lakini kwanza barani Afrika na kuongeza kwamba katika kufanikisha hilo, Israel inafungua ubalozi jijini Kigali, Rwanda.

Kwa sasa Balozi wa nchi hiyo anaishi Ethiopia akitoa huduma za kidiplomasia kwa nchi za Rwanda, Burundi na Ethiopia. Mwaka 2015 Rwanda ilifungua ofisi ya Balozi jijini Tel Aviv, Israel.

Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje, Ushirikiano na Mambo ya Afrika Mashariki wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe alisema, kufunguliwa kwa ubalozi wa Israel jijini Kigali kutaimarisha uhusiano baina ya nchi hizo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, ubalozi huo huenda utafunguliwa Juni- Julai mwakani. Kwa mujibu wa Waziri Nduhungirehe, pamoja na mambo mengine, ubalozi huo utaongeza fursa kwa wafanyabiashara wa Rwanda na Israel.

Waziri Nduhungirehe alisema ubalozi huo pia unatarajiwa kuwezesha kuanzishwa kwa safari za ndege kati ya Kigali na Tel Aviv. “Israel na Rwanda zimekuwa na uhusiano mzuri na zimeshirikiana kwenye mambo mengi.

Uamuzi wa kufungua ofisi umefanywa wakati mwafaka na utakuza ushirikiano,” alisema. Novemba 28 mwaka huu, Netanyahu alikwenda Nairobi, Kenya kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta na alizungumza na wakuu mbalimbali wa nchi za Afrika.

Wakati akizungumza kwenye Ikulu ya Kenya alisema, Israel iliomba kupewa hadhi ya kuwa mtazamaji kwenye Umoja wa Afrika (AU) kwa kuwa inataka kufanya kazi na Afrika.