Polisi Tanzania, Rwanda kukabili uhalifu pamoja

MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amesema jeshi lake litashirikiana na Jeshi la Rwanda katika kukabiliana na changamoto ya uhalifu wa makosa ya mtandao.

Sirro alitoa kauli hiyo jana wakati alipotembelewa na IGP wa Rwanda, Emanuel Gassana ili kuona maendeleo ya utekelezaji wa Mkataba wa Maridhiano baina ya jeshi la Tanzania na Rwanda.

Alisema suala la uhalifu wa makosa ya mtandao bado ni changamoto hivyo watakubaliana ili wawezekuwapeleka au kuwaleta wataalamu kwa ajili ya kupata elimu juu ya masuala la uhalifu wa mtandao na kuhakikisha wanawaongezea uwezo kuhusu masuala ya uhalifu wa mtandao.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kupitia mkataba wa makubaliano, Sirro alisema wameweza kupeana mafunzo kwa ajili kuwajengea uwezo askari, operesheni za pamoja na kubadilishana taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuzuia na kupambana na uhalifu baina ya nchi hizo.

Aidha Sirro alitoa tahadhari kwa wahalifu nchini wanaofanya matukio na kukimbilia Rwanda kuachana na tabia hiyo kwa kuwa majeshi hayo yanashirikiana katika utendaji kazi ikiwa ni pamoja na masuala yote ya kihalifu yanayofanywa na raia wa nchi hizo.

“Usifikirie utafanya tukio hapa uende Rwanda usikamatwe tunashirikiana kikamilifu katika msauala yote ya kihalifu niwaambie tu ni bora ukaachana na kazi hiyo ukafanya mambo mengine kwa sababu tukikukamata tutakuchukulia hatua na utaharibu maisha yako,” alisisitiza Sirro.

Kwa upande wake, Gassana alisema majeshi ya nchi zote mbili yamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika utendaji kazi lengo ni kuhakikisha nchi hizo zinakabiliana na vitendo vya kihalifu.

Alisema tangu wafikie makubaliano, wamekuwa wakifanya mambo mengi katika kuhakikisha wanakuwa na mafunzo hasa katika masuala ya uhalifu wa mtandao, ugaidi, biashara haramu ya binadamu pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya.